Karia : Lazima tupambane Yanga ifuzu CAF

Muktasari:

Yanga itaaikabiri Pyramids kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kabla ya kurudiana nchini Misri ambapo mshindi wa mechi hiyo atafuzu kucheza hatua ya makundi.

WAKATI keshokutwa Jumapili Yanga itashuka uwanjani kuikabiri Pyramids ya Misri katika mchezo wa kutafuta nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika, rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amesema watapambana kwa hali na mali kuisapoti Yanga ili Tanzania iendelea kupata nafasi zaidi uwakilishi wa timu nyingi kimataifa.
Msimu huu, Tanzania iliwakilishwa na timu nne kwenye Ligi ya Mabingwa na kombe Shirikisho Afrika baada ya Simba kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na kutolewa hatua ya robo fainali, matokeo ambayo yaliiongezea Tanzania pointi zilizoiwezesha kuingiza timu hizo.
Licha ya Simba msimu huu kuondoshwa mapema kama ilivyokuwa kwa KMC, Azam, Malindi na Mafunzo, Karia amesema wataelekeza nguvu kuisapoti Yanga ili kupigania pointi zitakazoiwezesha Tanzania kuendelea kuwa na uwakilishi wa timu nyingi CAF.
"Lazima tupambane Yanga iingie makundi, katika nchi ambazo zinagombea pointi hizo, washindani wetu pia wamo kama Gor Mahia ambaye naye hajatolewa kimataifa, lazima tupambane ili pointi zetu ziongezeke na tuendelee kuwa na timu sita kimataifa msimu ujao," alisema.
Alisema kwa kufanikisha hilo uongozi wa juu wa TFF kuanzia leo Ijumaa umepiga kambi jijini Mwanza kuhakikisha wanakuwa bega kwa bega na Yanga katika mchezo huo wa Jumapili.
"Tulikaa nao awali na baada ya kuamua mechi yao ikachezwe Mwanza, tulishauriana na bado tunaendelea kushirikiana kwa hali na mali, hii ni mechi ya Watanzania hivyo hatuna budi kuhakikisha tunashinda kama Taifa," alisisitiza Karia.