Kanuni mpya Ligi Kuu Bara timu nne kushuka daraja msimu huu

Muktasari:

Maboresho hayo ya kanuni hiyo, inamaana kwa msimu huu zitashuhudiwa timu nne moja kwa moja daraja la ambazo zitakuwa zitamaliza  kwenye nafasi ya  17, 18, 19  na 20, huku  timu mbili zilizoshika nafasi ya15 na 16  zikicheza mchujo na mbili za daraja la kwanza.

Dar es Salaam.  Wakati msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ukitarajiwa kuanza rasmi hapo Jumamosi kwa michezo minne kupigwa, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura ametangaza maboresho ya kanuni za ligi hiyo kwa msimu huu.

Wambura alisema kamati ya utendaji imepitisha kanuni   ambazo zitakazotumika msimu huu wa 2019/20, baada ya awali kukusanywa kwa mapendekezo ya wadau mbalimbali na kuyafanyia kazi.

“Kitu cha kwanza ambacho tumekifanyia kazi kwenye kanuni ni mabadiliko ni mfumo, tunarudi kwenye Ligi yenye muundo wa timu 16. Tunaenda na utaratibu wa kupunguza timu kila baada ya msimu kwa maana nyingine msimu wa 2020/21 tutakuwa na timu 18 msimu utakaofuata zitaopungua tena mbili,” alisema Wambura.

Maboresho hayo ya kanuni hiyo, inamaana kwa msimu huu zitashuhudiwa timu nne moja kwa moja daraja la ambazo zitakuwa zitamaliza  kwenye nafasi ya  17, 18, 19  na 20, huku  timu mbili zilizoshika nafasi ya15 na 16  zikicheza mchujo na mbili za daraja la kwanza.

Wambura alisema utaratibu wa kupanda Ligi Kuu kwa timu za daraja la kwanza utakuwa vile vile kwa vinara wa makundi yao mawili kupanda moja kwa moja huku watakaomaliza nafasi ya pili kwenye kila kundi wakicheza mchujo.

“Lakini baada ya msimu ujao kumalizika tutaondokana na mfumo wa kucheza makundi kwenye Ligi daraja la kwanza, watakuwa wakicheza ligi yao,” alisema.

Msimu huu Ligi Daraja la Kwanza (2019/20) zitashuka timu nane moja kwa moja ikiwa timu nne kila kundi timu ambazo zitakuwa zimeshika  nafasi ya 9, 10, 11 na 12 kwenye kila  kundi  itashuka moja kwa moja kwenda daraja kwa pili huku aliyeshika nafasi ya 7 na 8 watacheza mchujo na timu za daraja la pili.

Msimu wa (2020/21) Ligi daraja la kwanza zitashiriki timu 20 ikiwa timu 12 zilizobaki Ligi daraja la kwanza (sita kila kundi), timu nne ambazo zimeshuka daraja kutoka Ligi  Kuu, timu mbili ambazo zimepanda daraja kutoka ligi daraja la pili na timu mbili ambazo zitashinda michezo ya mchujo  kwa timu zilizoshika nafasi ya saba na nane  na zile mbili kutoka  Ligi daraja la pili.

Mtendaji huyo Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, alizungumzia vile walivyofanyia maboresho ya kanuni  ya utoaji wa adhabu uwanjani (kadi) kuwa safari itawahusu pia na makocha ambao wamekuwa wakikaa kwenye mabenchi  ya ufundi.

Pia alisema wameweka mkazo kwenye  kanuni ya usajili wa wachezaji wa kigeni  wenye vigezo maalumu kuwa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na vibali vya kuishi pamoja na kufanyia kazi.

Vigezo alivyovitaja kwa uchache ni pamoja na kuwa mchezaji ambaye amewahi kucheza timu yake ya taifa au atoke kwenye klabu ambayo inashiriki  Ligi  Kuu kwenye  taifa husika na kama aatokea Ulaya au Amerika na kwingineko, klabu anayotoka isiwe chini ya daraja la tatu.

Katika ufafanuzi wa kanuni hizo, Wambura alisema  benchi zima la ufundi  wanatakiwa kuwa na mavazi rasmi yaliyokidhi vigezo vya TFF ili kulinda hadhi ya ligi vilevile alisema  ili kocha aweze kufundisha timu inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara na ligi daraja la kwanza lazima awe na leseni ya ukocha kwanzia daraja B na kwa upande wa ligi daraja la pili  na la  tatu  Kocha anatakiwa awe na leseni ya ukocha kwanzia daraja C.

Pia alisema kila timu inatakiwa ifanye promosheni ya wachezaji wasiopungua watatu kutoka timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 na wenye umri chini ya miaka 17 ambao wamesajiliwa na TFF huku kila timu mwenyeji akiwajibika kuandaa gari maalum la kubebea wagojwa ‘Ambulance’.