Kanuni AFCON zaitega Serengeti Boys

Muktasari:

Kanuni hizo za mashindano hayo ziliifanya Serengeti Boys kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika Gabon mwaka juzi, licha ya kulingana idadi ya pointi na Niger waliofuzu nusu fainali na kukata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia.

Dar es Salaam. Kutobadilishwa kwa kanuni za mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 yatakayofanyika nchini Aprili, kunaipa kazi kubwa ya kufanya timu ya vijana wa umri huo ya Tanzania 'Serengeti Boys' ili kuepuka kile kilichofanywa na kaka zao mwaka 2017.

Kanuni hizo za mashindano hayo ziliifanya Serengeti Boys kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika Gabon mwaka juzi, licha ya kulingana idadi ya pointi na Niger waliofuzu nusu fainali na kukata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia.

Niger walifuzu kwa kigezo cha kupata matokeo mazuri dhidi ya Serengeti Boys katika mchezo baina yao, lakini pia walikuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga, kigezo cha pili cha kanuni za mashindano hayo ambacho hutumika kuamua mshindi iwapo timu mbili zimelingana pointi.

Kwa maana hiyo, Serengeti Boys inapaswa kuhakikisha inavuna matokeo mazuri kwenye mechi za hatua ya makundi ili kuepuka kulingana pointi na timu nyingine, kuzuia yasitokee yale yaliyotokea mwaka 2017.

Katibu mkuu wa kamati ya ndani ya maandalizi ya mashindano hayo, Leslie Liunda alisema hakuna mabadiliko ya kanuni katika fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo mwaka huu.

"Kanuni zitakuwa ni zile zile zilizotumika kwenye awamu iliyopita na hakuna mabadiliko ambayo yamefanyika," alisema Liunda.