Kane nje miezi miwili, kukosa mechi 11

Muktasari:

  • Hii inamaanisha Kane sasa atakuwa katika mbio za kujaribu kupona mapema na kuwepo katika pambano la kwanza la kihistoria la Tottenham katika uwanja wao mpya mnamo Machi 16 na wanatazamiwa kukipiga na Crystal Palace.

LONDON,ENGLAND.SIO tu kwamba Tottenham walichapwa na Manchester United nyumbani Wembley Jumapili usiku, lakini sasa imegundulika wamepata hasara kubwa zaidi ya kupoteza pambano hilo.

Staa wa timu hiyo, Harry Kane ambaye aliondoka anachechemea katika pambano hilo amefanyiwa vipimo na juzi imebainika atakaa nje kwa miezi miwili baada ya kuumia vibaya kifundo chake cha mguu katika pambano hilo.

Kane ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya England na inawezekana ndiye mchezaji muhimu zaidi Spurs kwa sasa, anatazamiwa kuwa nje kwa mechi 11 na hivyo kuipa timu yake wakati mgumu katika mbio za kuwania nafasi nne za juu pamoja na ubingwa wa EPL.

Juzi, Spurs walithibitisha staa huyo anatazamiwa kurudi mazoezini mwanzoni mwa Machi baada ya vipimo kuonyesha alikuwa ameumia vibaya wakati akiwania mpira na mlinzi wa United, Phil Jones katika pambano hilo Spurs walilochapwa 1-0. Hii inamaanisha Kane sasa atakuwa katika mbio za kujaribu kupona mapema na kuwepo katika pambano la kwanza la kihistoria la Tottenham katika uwanja wao mpya mnamo Machi 16 na wanatazamiwa kukipiga na Crystal Palace.

Kabla ya taarifa hiyo kuthibitishwa, mashabiki wa Tottenham walikuwa na hofu kutokana na picha za marudio kuonyesha staa huyo akitua vibaya na kukunja kifundo chake cha mguu ovyo huku majibu ya kitaalamu ya daktari yakionyesha atakaa nje kwa wiki nne hadi sita.

Baadhi ya mechi muhimu ambazo staa huyo anatazamiwa kukosa ni pambano la Jumapili ugenini dhidi ya watani wa jiji la London Fulham, pia atakosa pambano la marudiano la nusu fainali kombe la Ligi dhidi ya Chelsea Alhamisi ijayo ugenini Stamford Bridge baada ya Spurs kushinda mechi ya kwanza nyumbani Wembley.

Endapo Spurs watafanikiwa kutinga fainali Kane atalikosa pambano la fainali kombe la Ligi na Spurs wanalisaka taji la kwanza klabuni hapo tangu mwaka 2008 wakati walipotwaa taji hilo kwa kuichapa Chelsea mabao 2-1. Kuna uwezekano mkubwa mshindi wa nusu fainali akacheza na Manchester City.

Kane pia atalikosa pambano la kwanza la mtoano Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund mwezi ujao na kuna wasiwasi akalikosa pambano la marudiano litakalofanyika Machi 5 ikiwa ni siku ambazo anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi.

Kuna uwezekano pia Kane akalikosa pambano la watani wa jadi wa London Kaskazini dhidi Arsenal ambalo linatazamiwa kuchezwa Machi 2. Habari mbaya zaidi kwa Kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino mchezaji anayetakiwa kuziba pengo la Kane kwa kiasi kikubwa, Son Heung-min naye huenda asiwepo.

Kane anatazamiwa kuwa nje kuanzia Januari hadi februari na kukosa mechi tano zijazo za Spurs endapo timu yake ya taifa ya Korea Kusini itafika mbali katika michuano ya mataifa ya Asia.

Kwa sasa Pochettino analazimika kukuna kichwa kujua mchezaji ambaye ataziba pengo la ane ambaye msimu huu ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Tottenham kufunga mabao 20 kwa misimu mitano mfululizo.