Kane amtia hofu Michael Owen

Muktasari:

Spurs wanaamini staa wao huyo atakuwa nje ya uwanja hadi Aprili, lakini Jose Mourinho alisema straika wake huyo itamchukua muda mrefu kupona kuliko inavyotarajiwa.

LONDON, ENGLAND . MICHAEL Owen amekiri ana wasiwasi mkubwa juu ya afya ya straika Harry Kane haoni kama atakuwa fiti kucheza kwenye mikikimikiki ya Uero baadaye mwaka huu.

Straika huyo wa Tottenham Hotspur hataonekana uwanjani kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli aliyopata kwenye mchezo wa Mwaka Mpya dhidi ya Southampton.

Staa huyo amefanyiwa upasuaji na sasa anapambana kupona huku chama lake la England likitarajia kucheza mechi yake ya kwanza ya Euro 2020 dhidi ya Croatia, Juni 14.

Spurs wanaamini staa wao huyo atakuwa nje ya uwanja hadi Aprili, lakini Jose Mourinho alisema straika wake huyo itamchukua muda mrefu kupona kuliko inavyotarajiwa.

Mourinho alisema: “Tunamtarajia kurudi katikati ya Aprili, Mei au pengine msimu ujao, mi sifahamu.”

Maneno kama hayo ya Mourinho ndiyo yanayomtia shaka Owen kama mchezaji huyo atapona kwa wakati na kucheza kwenye Euro.

“Napata wasiwasi na kusema naona amepata majeraha kama yale niliyowahi kuyapata mimi,” alisema Owen.

“Nimesikia majeraha aliyopata ni kama yale niliyoyapata mimi. Kama atafanyiwa kama nilichofanyiwa mimi, basi hakuna uhakika wa kurudi Aprili.”