Kanda ya Ziwa Mguu sawa kwa Ligi Kuu

Muktasari:

Ligi Kuu na michezo mingine inatarajia kuanza Juni Mosi mwaka huu, ambapo timu zimeanza mikakati ya kurejea kambini kuanza mazoezi ya pamoja kujiandaa na mashindano hayo.

Mwanza. Wakati presha ya kuanza kwa Ligi Kuu ikiendelea kushika kasi, viongozi na makocha wa timu hizo wameeeleza namna wanavyojipanga kurejea uwanjani kwa kishindo.

Ligi Kuu na michezo mingine iliyokuwa imesimama kwa miezi miwili, inatarajia kuendelea Juni Mosi, huku timu zikitakiwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya virusi vya Corona.

Kocha Mkuu wa Alliance FC, Kessy Mzirai amesema kwa sasa benchi la ufundi wanasubiri utaratibu kutoka Bodi ya Ligi (TPLB) ikiwamo ratiba na mwongozo, huku akibainisha kuwa wako tayari kwa mapambano.

“Programu zipo tayari na wiki ya kwanza itakuwa ya uangalizi kwa vijana kujua wamekujaje, lakini siwezi kueleza nini naenda kufanya hadi hapo taarifa ya Bodi ya Ligi itakayoletwa ikiwamo ratiba” amesema Mzirai.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Klabu hiyo, Jackson Mwafulango amesema uongozi kwa sasa unapambana kuwaita wachezaji kambini na kwamba suala hilo linaendelea kutekelezwa.

“Kwanza tuliwaambia benchi la ufundi kuwasilisha mahitaji yote, lakini kama haitoshi uongozi tutakuwa na kikao cha ndani Jumapili kuweka mikakati ili kuhakikisha Jumatatu wachezaji wote wanakuwa kambini” amesema Mwafulango.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema wao wako tayari na anaamini vijana watakuja kwa kasi ile ile na kama kutakuwa na vitu vya kuongeza, benchi la ufundi limejipanga.

“Hata Ligi ianze leo au kesho, hakuna tatizo sisi tuko tayari na ninaamini kasi yetu itakuwa ileile, ninachofikiri hata kama kutakuwa na mapungufu tutayafanyia kazi” amesema Maxime.

Mratibu wa timu hiyo, Paul Ngalyoma alisema mikakati yao inaenda vizuri na zaidi kila kitu kitawekwa wazi baada ya wachezaji kufika kambini na kwamba uongozi umejipanga kimkakati.

“Hadi sasa hakuna tatizo kimsingi tunawasiliana na wachezaji mmoja mmoja kuhakikisha baada ya siku kuu wote wanakuwa pamoja ili kuanza rasmi program, kiufupi tumejipanga” amesema Ngalyoma.

Naye Kocha Mkuu wa Biashara United, Francis Baraza amesema baada ya taarifa za kurejea kwa Ligi, wanatarajia kuingia tena kambini Jumanne na kuwataka wachezaji kuheshimu kazi yao na mikataba.

“Jumanne ndio siku tumepanga kuingia kambini na tayari kuna baadhi ya wachezaji ambao wameanza kuingia wale wa karibu, sitaki kupoteza muda naamini kila mmoja anaelewa umuhimu wa mkataba wake” amesema Baraza.

Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Seleman Mataso ameliambia Mwanaspoti Online kuwa mipango yao inaenda vizuri na kwamba wanahitaji kuendeleza moto wao haswa kwa kushinda mechi zote za nyumbani.

“Wachezaji wote wameshapewa taarifa na utaratibu wa kurejea kambini, uongozi umejipanga vizuri kuhakikisha ule moto wetu unaendelea ikiwamo mechi za nyumbani kushinda zote” amesema Kigogo huyo.