Kambi mpya Yanga hii hapa

KAMA hukuiona Yanga katika kilele cha wiki ya Mwananchi, basi utalazimika kuwaona tena mjini Septemba 6 katika ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu Bara, hiyo ni baada ya tajiri wao mmoja kuihamisha timu nzima.

Iko hivi. Mpaka jana asubuhi Yanga ilipata kifungua kinywa katika Hoteli ya Regency Park, Mikocheni lakini mchana wakahamishwa na Bilionea wa GSM, Ghalib Mohamed ili wapate maandalizi yenye utulivu tayari kwa kuanza msimu mpya.

Tajiri huyo ambaye hapendi kuzungumza sana, ameipeleka Yanga eneo la Kigamboni na kama unatoka Posta mpya jijini Dar es Salaam kisha ukavuka na kivuko ni umbali wa kilomita zisizopungua 29 kufika ilikofichwa Yanga wakiwemo mastaa wao wapya, mshambuliaji Michael Sarpong na winga Tuisila Kisinda.

Yanga imewekwa kwenye majengo maarufu ya Avic yaliyojitenga na yenye utulivu mkubwa na vifaa kibao vya michezo ukiwemo uwanja wa ndani kwa ndani na hakuna mgeni anayeruhusiwa kuingia ndani bila ruhusa maalumu.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya Yanga, tajiri huyo ameamua itakuwa inaishi hapo kuanzia sasa na hakuna habari ya hotelini tena kwani hapo ni pazuri zaidi na kocha amepakubali.

Ukifika eneo hilo unakutana na ukuta mrefu na ndani yake tena kuna ukuta mwingine uliopishana kama nusu kilomita na ndani ya ukuta wa pili ndio kuna majengo mbalimbali ya makazi mapya ya Yanga.

Jana mchana Mwanaspoti lilishuhudia kikosi hicho kikiingia katika nyumba ya tajiri Ghalib Mohamed kisha kupata chakula cha mchana wakiwa humo na baadaye kurudi katika majengo yao.

KOCHA AFUNGUKA

Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic amesema timu hiyo inahitaji angalau mwezi mmoja ili icheze kwa kiwango anachotaka huku akiwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango bora katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Aigle Noir ya Burundi.

Zlatco alisema wachezaji wake walijitahidi ingawa bado hakuna muunganiko na wataitumia wiki moja iliyobaki kurekebisha mapungufu kabla ya kuanza kwa Ligi Septemba 6.

“Ninachowaahidi hapa kwangu ni kazi na nidhamu, huo ndio mwongozo wangu,” alisema Zlatko na kuongeza, Yanga inahitaji mazoezi zaidi ili kutengeneza muunganiko mzuri na icheze kwa ubora mkubwa.

“Si kazi rahisi kupata muunganiko wa timu kwa muda mfupi hivi, ukizingatia timu ina wachezaji 14 wapya, hivyo inahitaji muda ili kuzoeana.

“Licha ya kwamba muda ni mfupi, tutatumia wiki moja iliyobaki kuyafanyia kazi mapungufu yetu ili tuanze vizuri ligi, lakini ili timu icheze kwa ubora wake inaweza kuchukua mwezi mzima ili kuwafanya wachezaji wote kuzoeana na kucheza kwa maelewano,” alisema Zlatko.

“Nimewaangalia wachezaji wote waliosajiliwa wana vipaji vikubwa, hivyo muhimu wanatakiwa kujitoa kwa ajili ya timu na kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja,” alisema Zlatko.