Kamati TFF bado yasaka leja ya Yanga

Saturday December 8 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

HADI jana Ijumaa, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ikimaliza mchakato wao wa usaili wa wagombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Yanga, ilikuwa haijapata leja ya wanachama wa klabu hiyo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Januari 13 mwakani ukisimamiwa na Kamati hiyo baada ya upande wa Yanga kushindwa kutoa ushirikiano kuanzia hatua ya awali ya mchakato huo.
Kamati hiyo ilianza usaili wa wagombea hao tangu juzi Alhamisi ambapo walilazimika kutumia barua za uthibitisho kutoka kwenye matawi ya wagombea hao ambazo zilitakiwa kusainiwa na Wenyeviti ama Makatibu wa matawi husika.
Hata hivyo, wagombea wengi waliofika kwenye usaili huo hawakuwa na barua hizo zaidi ya kadi za uanachama ambapo walitakiwa kupeleka barua hizo ama kuzituma kwa njia ya mtandano.
Wagombea hao bila kutajwa majina waliliambia Mwanaspoti ambalo lilipiga kambi kwenye ofisi za makao makuu ya TFF kwamba, awali hawakuambia juu ya barua hizo lakini juzi hiyo hiyo ndiyo walitakiwa kuwa na barua.
"Sio tatizo kubwa, tutakwenda kuchukuwa barua kama walivyotuagiza, kila mtu aliyefika hapa amefanyiwa usaili bado hiyo barua tu iliyotakiwa," alisema mgombea huyo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ally Mchungahela alisema kuwa; "Leja hatujapata lakini sio tatizo kwetu, tutaipata muda wowote, kuhusu barua kila aliyesailiwa amekuja na barua wale ambao hawakuwa na barua tumewaagiza wazilete kabla ya Ijumaa (jana) ambayo ndiyo siku ya mwisho ya usaili wetu,"
Juzi jumla ya wagombea 13 walisailiwa huku wengine wakibaki wagombea 10 ambao jana walitarajiwa kusailiwa na leo Jumamosi majina yaliyopitishwa yatatangazwa.

Advertisement