HISIA ZANGU: Kama wachezaji wa Azam wangevaa jezi ya Yanga

SIMBA imechukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Hadithi imekwisha. Mpaka tunavyozungumza Yanga wanashika nafasi ya pili. Na kuna uwezekano mkubwa wakamaliza katika nafasi hiyo. Azam haipati matokeo mazuri.

Hivi karibuni walidhulumiwa pointi zao dhidi ya Yanga lakini wakaenda mikoani na kuvurunda zaidi. Wamefika maji ya shingoni. Nikiitazama timu yao ni nzuri. Wachezaji wao wote wangeweza kuingia katika kikosi cha kwanza cha Yanga.

Wakati watu wakikumbuka kuwa Azam zamani ilikuwa na mastaa wakubwa kama akina Kipre Tchetche na John Bocco, nakukumbusha tu kwamba hata Azam hii ina mastaa wengi wakubwa. Wengi. Kulia kuna Nicolas Wadada, mlinzi bora wa upande wa kulia katika Ligi yetu.

Kushoto kuna Bruce Kangwa. Katikati kuna akina Yakub Mohamed na Agrey Morris. Mbele pia kuna akina Shaban Chilunda, Never Tegere, Richard Djodi na wengineo. Kwanini wanashindwa kuipa wakati mgumu Simba?

Hata wakati Azam ikiwa imetimia, ilitwaa mara moja tu ubingwa wa bara. Simba wakaunda timu yao na sasa wamechukua mara tatu. Hata sasa Yanga wanaweza kuunda timu yao na kuiacha Azam ilipo na wakachukua ubingwa wa Ligi Kuu.

Tatizo ni nini? Azam kuna mambo mawili yanawakaba. Kubwa zaidi ni ukweli kwamba wachezaji wao hawapati presha kubwa kutoka kwa mashabiki. Hauwezi kusikia mchezaji wa Azam anazomewa na mashabiki wa Azam.

Mchezaji wa Azam anazomewa akija uwanja wa Taifa kucheza na Simba au Yanga. Na hatazomewa na mashabiki wa Azam. Atazomewa na mashabiki wa Simba au Yanga kutegemeana na mashabiki wanaozomea wanataka nini kwake.

Mashabiki wa Simba wanaweza kumzomea Abubakar Salum katika pambano dhidi ya Yanga. Kisa? Watahisi anacheza kinazi kwa sababu baba yake alikuwa staa wa zamani wa Yanga, Salum Abuubakar. Upande mwingine inaweza kuwa hivyo hivyo tu.

Mashabiki wa Yanga wanaweza kumzowea Shaban Chilunda kama akikosa mabao mawili matatu. Wanaweza kumuhusisha na Simba wenyewe. Hata hivyo ni nadra kwa mchezaji wa Azam kuzomewa na shabiki wa timu yake. Hapo hapo jiulize, mashabiki wenyewe wa dhati wanao?

Kikubwa kwa Azam ni kwamba timu haina moyo wake. Wachezaji hawa hawa ukiwapeleka Yanga wanaweza kuipa ubingwa na kuifanya itambe ukanda huu wa Afrika mashariki na kati. Wataipata presha ambayo hawajawahi kuipata maishani.

Kwa mfano, leo kuna mashabiki wa Simba wanaamini kwamba Aishi Manula anafungwa sana mabao ya mashuti ya mbali. Jiulize, mashabiki walikuwa hawafahamu hili wakati akicheza Azam? hapana, walikuwa hawamfuatilii.

Leo John Bocco akikosa mabao ya wazi mashabiki watamuweka katika presha kubwa. Alipokuwa anakosa mabao hayo Azam kulikuwa hakuna wa kumuuliza. Alipowahi kukosa mabao ya wazi akiwa na timu ya taifa wakati ule akiwa mchezaji wa Azam alitukanwa mpaka akatangaza kutoitaka tena Stars.

Pale alikumbana na mashabiki wenye presha ambao walimuweka katika presha ambayo hakuwahi kukumbana nayo klabuni. Ni kitu cha kawaida kwa timu hizi. Unahitaji roho ya chuma. Na hii presha ndio ambayo Yanga wameipeleka kwa Yikpe kwa sasa. Ni mchezaji gani wa Azam amewahi kuwekwa katika presha kama ile? Hapa ndipo kuna ugumu na changamoto za kuchezea timu hizi mbili za Kariakoo. Lakini ni presha ambayo baadaye inazaa matunda. Inamfanya mchezaji apambane.

Kama Azam wanataka kujitofautisha zaidi basi waanze kununua mastaa wakubwa zaidi ya hawa walionao. Binafsi naamini walionao wana uwezo wa kufanya kitu kama wangekuwa wanawekwa kikaangoni. Lakini labda wapandishe daraja zaidi, kitu ambacho sikitegemei.

Azam hawajataka kwenda katika uwekezaji wa akina Al Ahly, Esperance, Zamalek, Raja Casablanca na wengineo. Ndio maana hawajawahi kununua wachezaji wa dola 500,000 ingawa uwezo huo wanao.

Labda wakienda katika uwekezaji huo watapandisha daraja zaidi la wachezaji wao na watatwaa ubingwa kiurahisi.

Pale Afrika Kusini, Mamelodi Sundown ni timu ambayo haina mashabiki wengi kama ilivyo kwa timu za asili, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates. Hata hivyo kiwango chao cha uwekezaji kimekuwa kikubwa kiasi kwamba timu za wananchi zimekwama kufikia ubora wao. Labda Azam wafanya hivyo.

Hata hivyo sioni Azam ikifanya hivyo na badala yake wanalazimika kutumia mastaa walionao kuifanya kazi hiyo. Kwa mastaa hawa sina shaka na viwango vyao lakini kama wangekuwa wanavaa hizi jezi za timu za Simba na Yanga huenda hadithi ingekuwa tofauti.

Ukiwauliza akina Bocco, Erasto Nyoni, Aishi Manula na Shomari Kapombe tofauti ya kucheza Simba na Azam watakwambia. Watakwambia namna ambavyo mahitaji ya ushindi kwa Simba ni makubwa zaidi.

Wakati mwingine mchezaji mwingine anaweza kusikia raha zaidi kucheza Azam kuliko Simba na Yanga kwa sababu anataka kukaa sehemu salama ambayo hatapata misukosuko. Hata hivyo mchezaji akihitaji nafuu hiyo ujue timu haiwezi kusonga mbele. Tazama jinsi ambavyo David Molinga alijibu mapigo baada ya kuzomewa hivi karibuni. Moyoni alipania kufanya kitu katika pambano dhidi ya Namungo kwa ajili ya kujibu mapigo ya mashabiki. Na kweli. Hasira zake zilimsaidia yeye mwenyewe na ziliisaidia timu kupata matokeo katika pambano hilo gumu.

Siamini kama wachezaji wa Azam wanaishi hivi. Haitoshi kupata hasira kutoka kwa maneno ya matajiri wa timu pekee. Inabidi ucheze kwa ajili ya jukwaa. Sio tu kwa mechi za Simba na Yanga. Kwa kila mechi inayokuja usoni. Ubingwa haupatikani kwa kuzifunga Simba na Yanga pekee.