Kama sio Kagere, basi ujue ni Chama

BAADHI ya nyota wa zamani wa soka nchini wameiangalia orodha ya wachezaji 30 iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu na kuweka turufu yao kwa mastaa wawili wa Simba wakidai kama sio Meddie Kagere basi ni lazima awe Clatous Chama.

TFF ilitoa orodha hiyo ya wachezaji 30 wa Ligi Kuu ya msimu huu iliyomalizika wiki iliyopita na kusema watachujwa kupata watatu watakaoingia fainali na kupata mmoja anayestahili kubeba tuzo hiyo kwa msimu huu, hata wakongwe wa soka nchini wametoa maoni yao na kuwataja kina Kagere kuibeba.

Wakizungumza kwa muda tofauti, nyota wa zamani wa kimataifa, Zamoyoni Mogella alisema kwa upande wake anampa Kagere kutoka na idadi yake ya mabao aliyonayo mpaka ligi inamalizika.

“Kagere ndiye mfungaji bora wa msimu hawezi kukosa katika nafasi tatu za juu, Chama naye ni mchezaji ambaye ameonyesha uwezo mkubwa kwa timu yake na pia kwa mchango wake binafsi na wa tatu ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga alikuwa bora sana licha ya timu yake kutofanya vizuri,” alisema Mogella aliyezichezea Simba na Yanga sambamba na Taifa Stars mbali na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Naye nyota wa zamani wa timu hizo, Edibily Lunyamila aliweka karata zake kwa Chama, Kagere na Feisal Salum akidai mmoja wao anaistahili kwa msimu huu kwa kazi kubwa waliyofanya.

Lunyamila alisema, amewachagua nyota hao kutoka nyota 30 waliotangazwa kutokana na mchango wao binafsi na pia msaada wao katika timu zao.

“Wachezaji wote waliochaguliwa ni wazuri sema wanapishana tu kidogo michango yao ndani ya timu lakini hao niliowataja kwangu mimi naona wanafaa kuingia tatu bora ya kumpata mshindi,” alisema Lunyamila aliyewahi pia kuichezea Malindi na Biashara Shinyanga, huku Mfungaji Bora mwenye rekodi yake, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alimtaja Chama, Feisal na Awesu Awesu wa Kagera Sugar.

“Nimewachagua hao watatu kutokana na mchango wao na uwezo wao katika kuisaidia timu, hao niliowaacha sio kusema hawana uwezo hapana naona hao ni bora zaidi yao,”

Kwa upande wa kipa wa zamani wa kimataifa, Idd Pazi “Father’ alisema karata yake anaitupa kwa Chama akidai alichangia kwa asilimia kubwa timu yake kupata matokeo mpaka kutwaa taji la Ligi mara tatu mfululizo, pia akimchagua Deus Kaseke wa Yanga akidai licha ya timu hiyo kutofurukuta zaidi, ila ilipofikia mchango wake ni mkubwa na karata yake ya tatu ni kwa Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar.

Katika orodha iliyotangazwa na TFF ina wachezaji Shomary Kapombe, John Bocco, Meddie Kagere, Clatous Chama, Francis Kahata, Jonas Mkude, Luiz Miquissone na Aishi Manula.

Yanga ni Feisal Salum, Mapinduzi Balama, Deus Kaseke, David Molinga na Juma Abdul, Birigimana Blaise, Lucas Kikoti na Reliants Lusajo (kutoka Namungo), David Luhende, Awesu Awesu, Yusuph Mhilu (Kagera Sugar), Martin Kigi (Alliance), Daruwesh Saliboka (Lipuli) na Marcel Kaheza (Polisi Tanzania).

Wengine ni Nico Wadada, Idd Seleman ‘Nado’ na Obrey Chirwa (kutoka Azam), Abdulmajid Mangalo, Daniel Mgore (Biashara United), Ayoub Lyanga na Bakar Mwamnyeto (Coastal Union) na Waziri Junior (Mbao Fc).

Nyota hao watafanyiwa mchujo ili kubaki 10 kabla ya kupata tena watatu watakaoingia fainali ya kutoa mshindi katika sherehe za tuzo za VPL zitakazofanyika Ijumaa katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam zitakazoambatana na hafla ya kuwazadiwa washindi wengine wa msimu wa 2019-2020.