Kama pesa ipo! Ligi ya England inakwama wapi?

Muktasari:

Msimu ujao sasa, timu hizo zimeboresha vikosi vyao, wakisajili wachezaji mahiri na makocha bora. Tena wachezaji iliyowasajili na makocha iliyowabeba, wengine wametoka kwenye Ligi Kuu England.

LIGI Kuu England wanakwama wapi sijui. Dili za televisheni zinaleta pesa nyingi kwenye klabu zao, lakini bado wanakwama. Pesa si ndo kila kitu?

Wanahofia kutumia? Au hawana watu mahiri kwenye kukamilisha dili zao? Nazungumzia usajili. Ligi Kuu England inafeli mara nyingi linapokuja suala la kufukuzia wachazaji mahiri wa kuwasajili na ligi nyingine.

Ona wanashindwa hadi na Serie A mahali ambako wachezaji wanaolipwa mshahara wa kuanzia Pauni 200,000 kwa wiki ni wa kuhesabu. Wanakwama wapi?

Cheki ishu ya Joao Felix. Tazama hii ya Mat de Ligt. Wawili hao kwa muda mrefu kwenye kipindi hiki cha dirisha la usajili huko Ulaya, wamehusishwa sana na klabu za Ligi Kuu England, tena wababe kabisa kuanzia Manchester City, Manchester United na Liverpool, lakini hakuna hata moja iliyofanikiwa kunasa huduma zao, wamenaswa huko La Liga na Serie A.

Felix ametua Atletico Madrid na De Ligt yupo zake Juventus. Tena wamenaswa kwa pesa ambazo zisingekuwa tatizo kwa klabu za England. Jambo hili ndilo linalowafanya wawe wanasubiri kwa muda mrefu kutamba kwenye soka la Ulaya.

Antoine Griezmann amehusishwa sana na Ligi Kuu England, lakini amebaki kwenye La Liga, akiondoka Atletico na msimu atakuwa Nou Camp kukipiga na Lionel Messi kwenye kikosi cha Barcelona.

Msimu uliopita, Ligi Kuu England ilitamba kwenye michuano yote mikubwa ya Ulaya, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League. Lakini hilo limekuja baada ya vikosi vya timu kama Real Madrid, Barcelona, Juventus, Bayern Munich kutokuwa kwenye ubora wao.

Msimu ujao sasa, timu hizo zimeboresha vikosi vyao, wakisajili wachezaji mahiri na makocha bora. Tena wachezaji iliyowasajili na makocha iliyowabeba, wengine wametoka kwenye Ligi Kuu England.

Staa wa medali ya ushindi ya Europa League, Eden Hazard ameondoka Chelsea kwenda kujiunga na Real Madrid, wakati aliyekuwa kocha wake huko Stamford Bridge, Maurizio Sarri amekwenda zake Juventus.

Hapo Ligi Kuu England imeshindwa kuwalinda watu wake makini wasiondoke. Imeshindwa kufanya hivyo kwa miaka mingi. Ilimwaacha Cristiano Ronaldo aondoke.

Gareth Bale, Luka Modric, Philippe Coutinho, Luis Suarez, Cesc Fabregas, Dimitri Payet, Arjen Robben, tena wote waliondoka wakiwa kwenye ubora wao. Ni kama kilichotokea tu kwa Hazard.

Utashangaa, ligi yenye pesa nyingi, lakini yenyewe itashinda kunasa wachezaji wale tu ambao hawatakuwa kwenye ushindani na ligi nyingine. Karim Benzema, Ronaldinho, Ricardo Kaka, Messi, Zinedine Zidane, hii leo wangekuwa kwenye historia ya kucheza kwenye Ligi Kuu England, lakini walishindwa kukamilisha dili za kuwabeba na wakanaswa na ligi nyingine.

Hivi ndivyo Ligi Kuu England inavyowafelisha mashabiki wake kupata fursa ya kuwaona mastaa bora kabisa kwenye soka wakicheza kwenye ligi hiyo. Nani ambaye asingependa kumwona Messi au Ronaldinho akicheza kwenye Ligi Kuu England? Hakuna.

Arsene Wenger na mpinzani wake Sir Alex Ferguson walikuwa na nafasi ya kuwaleta wakali kwenye Ligi Kuu England wakashindwa kukamilisha dili. Tatizo.

Jambo hili linawafanya wasiwe ligi inayotoa washindi wa Tuzo ya Balon d’Or. Mchezaji wao wa mwisho kubeba tuzo hiyo ni Ronaldo, na tangu aondoke Old Trafford kwenda Santiago Bernabeu mwaka 2009, miaka 10 sasa England imetoka kapa kwenye Balon d’Or.

Na kwa staili yao ya usajili, kushindwa kubeba watu wa kazi, watasubiri sana.

Mwaka huu Virgil van Dijk anapigiwa debe, lakini tatizo kuna Ronaldo na pengine Messi, watatibua kila kitu. Tabu itabaki palepale.

Baada ya miaka michache mbele Van Dijk ataondoka. Hilo pia litawahusu mastaa wengine kama Mohamed Salah, Paul Pogba, Pierre Emerick Aubameyang, Alexandre Lacazette, Harry Kane, Dele Alli na Christian Eriksen.

England itaanza moja, kisha watafuata kila Marcus Rashford, Anthony Martial na David de Gea nao kuondoka. Baada ya hapo, Jurgen Klopp, Pep Guardiola, Unai Emery nao wataondoka.

Itakuwa ligi nyepesi, ambayo itapotea kwenye ligi za Ulaya kama ilivyokuwa miaka ya hapo kati. Ferguson alipoondoka na Wenger alipochoka akili.

England sijui wanakwama wapi, maana pesa wanayo nyingi hadi wanawalipa wachezaji kama Mesut Ozil, Rashford, Jesse Lingard, Alexis Sanchez mishahara ya kufuru ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine labda kwenye Ligi ya China tu, wanafeli wapi kuwanasa kina Neymar waje kuifanya EPL kuwa ligi bora zaidi duniani?