Kama hivyo, Messi wa nini?

Muktasari:

  • Lionel Messi amekosekana kwenye mechi kadhaa za Barcelona ikiwemo ya juzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa San Siro, na alikuwa Malcom aliyeingia kipindi cha pili na kufunga bao hilo lililoivusha timu hiyo.

PARIS, Ufaransa.KAMA ulishika kichwa baada ya kumwona Lionel Messi akiumia mkono, ukasema Barcelona ndio basi tena, utakuwa umenoa.

Barcelona ilifanya ‘advataizi’ ya kwanza kwenye El Clasico, Real Madrid ililala 5-1, ikawa historia bila Messi na juzi usiku ikafanya tena mambo, imeingia 16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya bila Messi kuwepo.

Barcelona imekuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutoka sare ya 1-1 na Inter Milan, huku Harry Kane akiiokoa Tottenham Hotspur wakati Liverpool imepoteza kete yake.

Mechi ya nyumbani, Liverpool iliilaza Red Star Belgrade, lakini kati ya yote, vijana wa Thierry Henry, Monaco, walitolewa kwenye mtifuano huo baada ya kuchakazwa na Club Brugge.

Lionel Messi amekosekana kwenye mechi kadhaa za Barcelona ikiwemo ya juzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa San Siro, na alikuwa Malcom aliyeingia kipindi cha pili na kufunga bao hilo lililoivusha timu hiyo.

Hata hivyo, Inter ilipata bao lake kupitia kwa Mauro Icardi dakika ya 87 lililokuwa la kusawazisha, na kuwafanya mabingwa hao wa Ulaya mara tatu kuungana na Barcelona kwenye 16 Bora kutoka Kundi B.

Tottenham bado inahaha, licha ya Harry Kane kuiwezesha kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya PSV Eindhoven. Waholanzi hao walicheza soka ya kuvutia uwanjani Wembley, na ndio waliokuwa wa kwanza kufunga baada ya Luuk de Jong kufyatua kombora la dakika ya pili tu. Vijana wa Mauricio Pochettino. Kane alisawazisha dakika ya 12 kabla ya kabla ya kufunga la pili dakika ya 89.

“Tulilazimisha kucheza kwa nguvu zote ili kupata matokeo. Kwa msimu mzima tumekuwa tukihangaika kupata matokeo,” alisema Kane.

Liverpool ilitisha zaidi ya Red Star lakini ililazwa huko Serbia, kwa kushindwa kihimili vishindo na kupigwa mabao 2-0 kama ilivyokuwa mwaka 1991 walipowafungwa kwenye Kombe la Washindi Ulaya. Straika wa Milan, Pavkov alifunga mara mbili dakika saba za kwanza katika mchezo huo, kwa kumzidi maarifa kipa Alisson kwa shuti kali.

“Imewachanganya wachezaji, imeniuma na inatakiwa tufanye vizuri zaidi kufikia mafanikio,” alisema Klopp.

Kupoteza mchezo huo kwa vijana hao wa Anfield ni wazi kumetishia uhai wao wa kusonga mbele kwenye Kundi C ambalo pia Napoli ilisawazisha bao na kufanya matokeo kusimama 1-1 dhidi ya Paris Saint-Germain usiku wa juzi.

Napoli iliikamata PSG

Kylian Mbappe alimtengenezea Juan Bernat mpira safi na kuifungia Paris bao la kuongoza dakika chache kabla ya mapumziko lakini Lorenzo Insigne alimtungua Gianluigi Buffon kwa mkwaju wa penalti ya kipindi cha pili.

“Hili ni kundi gumu, na kwa Liverpool kupoteza ni wazi lolote linaweza kutokea,” alisema mchezaji wa PSG, Julian Draxler. “Sare ya Naples si mbaya hivyo hatma yetu iko mikononi mwetu.”

Liverpool na Napoli zina pointi sita kila moja baada ya mechi nne, pamoja na PSG ina pointi moja nyuma wakati Red Star ikifuatia. Liverpool itaifuata PSG pambano linalofuata wiki ijayo.

Wakati huo huo, Atletico Madrid ililipa kisasi cha kufungwa mabao 4-0 ilipifungwa na Borussia Dortmund lakini juzi usiku vijana wa Diego Simeone walizinduika na kuwalaza mabao 2-0 mechi iliyochezwa Hispania, Saul Niguez na Antoine Griezmann ndio waliowatia njaa wapinzani wao.

Timu mbili za Kundi A bado hazina uhakika wa kuingia hatua ya 16 Bora, hata hivyo Club Brugge yenyewe ilishinda 4-0 dhidi ya Monaco.

Wabelgiji hao hawajatwaa ubingwa tangu 2005, lakini walikuwa mbele kwa mabao 3-0 kipindi cha kwanza mechi iliyopigwa Stade Louis II. Hans Vanaken alifunga mara mbili, ikiwemo bao la penalti, na Mbrazil, Wesley akafunga la tatu kabla ya Ruud Vormer kumalizia kazi kwa kufunga bao la nne.

Wasiwasi kwa Henry

Monacco iliyoingia nusu fainali 2017, ndio kwaheri. Ilikuwa siku mbaya zaidi kwa timu hiyo ambayo ilipoteza mechi 15 ikiwemo mechi tano mfululizo chini ya Henry.

Matokeo hayo yamekuja ikiwa ni siku moja baada ya bilionea wa klabu hiyo raia wa Russia, Dmitry Rybolovlev kukamatwa kwa rushwa na anashikiliwa kwa mahojiano.

Nayo FC Porto imewasha taa ya kijani kuelekea kufuzu kutoka Kundi D baada ya kuibandua 4-1 Lokomotiv Moscow. Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kuwa mbele kwa pointi mbili zaidi ya Schalke ambayo nayo iliichuna Galatasaray 2-0 mjini Gelsenkirchen.