Kalamu nyeusi ya Mtoto wa Mkulima: Nenda Shija msalimie mzee Richard

Muktasari:

Napata shauku ya kutaka kujua huko wanapokwenda hasa kunani, maana wanataja jina halafu wote wanakimbilia sehemu moja, nami nikaungana nao kuelekea huko walipokuwa wanaelekea wao.

Kelele zilipenya vyema sana kwenye ngoma za masikio yangu, hata zikanifanya nikurupuke kutoka kwenye kiseto kizito cha usingizi.

Sikujua kelele hizi hasa zinahusika na nini, shauku ya kutaka kuliju hilo likaniingia, wala sikufanya ajizi, nikakurupu kutoka kwenye godoro langu kuu kuu, na kutoka nje.

 Nilistaajabu ya Musa baada ya kuyaona ya Firauni, kwani nilishuhudia kundi kubwa watu la likiwa linakimbilia sehemu moja, huku wakiwa wanalitaja jina la aliyewahi kuwa Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Shija Richard. Napata shauku ya kutaka kujua huko wanapokwenda hasa kunani, maana wanataja jina halafu wote wanakimbilia sehemu moja, nami nikaungana nao kuelekea huko walipokuwa wanaelekea wao.

Safari ile ilikoma kwenye kiwanja kikubwa cha mpira, kinacho patikana maeneo ya Mbagala Kilungule, kilomita chache tu kutoka kwenye makazi ya Mheshimiwa Diwani wa eneo hilo, Said Fella, baada ya kufika kwenye kiwanja hiko, hakika nilitaharuki na kupata kigagaziko cha macho, juu ya mamia ya watu waliokuwepo hapo kwenye eneo hilo, sikujua hasa hata kilichofuatwa hapo ni nini, lakini niliendele kuenzi kauli ya marehemu Babu yangu kuwa , mvumilivu hula mbivu.

Nilikaa kimya nakusubiri kuangalia nini ambacho kinakwenda kujiri katika eneo hilo. Baada ya muda nikasikia sauti kutoka kwenye kipaza, iliyokuwa inawataka watu waliokusanyika hapo watulie, watu wote wakatulia tuliii kama kuku aliyechinjwa. Mara nikaanza kusikia waraka unasomwa, waraka ambao ulinifanya nitulie kuusikiliza kama Hakimu anayesikiliza kesi Mahakamani.

Wakala ulisikika ukisomwa kama ifuatavyo

“Ndugu wana Yanga wenzangu, akuambiae usikombe mboga sikuzote anataka ushibe, nani kasema usiku mmoja auozeshi nyama huyu, tumgeukie mara mbili na kumtazama, maana ametudanganya, nimeamuwa kukaa pembeni ili kuondoa makelele na migogoro kwenye timu, nafikiri wakati ndio utaongea, kama nani alikuwa sahihi na nani alikuwa Jahiri”

Waraka ule ulimalizika hivyo na baada ya hapo hakuna mtu yeyote aliyenong’ona, wala kuguna watu wote walitimka eneo hilo. Shida ilikuwa kwangu maana bado nilikuwa nautafakari waraka ule wa Shija ulioniacha mdomo wazi, waraka ambao ulinogeshwa na mashairi ya msanii maarufu hapa nchini, Mrisho Mpoto.

Moyoni nikawaza kuwa ivi ni mimi tu ambaye nimeona umuhimu wa kulijadili tukio la Shija kujiuzuru kwa kina? Kimsingi Shija hakujiuzuru tu, ili mradi aache uongozi Yanga, lakini amejiuzuru ili kuwafanya wana Yanga watafakari wanakoelekea, huenda hakutaka kuwa sehemu ya historia wakati Yanga inaanguka kutokana na hili wanalolitaka sasa hivi.

Lakini upande wa pili wa moyo wangu unanambia kuwa Shija ni mmoja ya watu walio kwenye kamati ya kodi ya majengo, ambao bado waamini ili wasogeze maisha yao basi lazima wapate chochote kitu, kutoka kwa Yanga na sio Yanga ipate chochote kitu kutoka kwao. Lakini bado hoja hii inakuwa dhaifu na kitendo cha yeye kuamau kujiuzuru kwani, huenda angeogopa kufanya hivyo kwakuwa angehofia maisha bila ya kodi hizo.

Kimsingi Shija alijiuzuru kwa hoja yenye mashiko sana , japo bado wana Yanga wamefumba macho na kuziba masikio kutotaka kusikia hili, Yanga mnahitaji kujitafakari sana na hiki kinacho endelea kwenye klabu yenu na ushauri wangu ni kwamba iwapo mnataka kumuona GSM akiwa anaendelea kubaki hapo, basi mfanyeni aweze kuingia kwenye mfumo rasmi, na sio hiki ambacho kinafanyika, maana mifano hai mnayo wenyewe juu ya kile kilichowakuta kwa Manji na mmeona hatari iliyokuwa inataka iwakumbe hapa baada ya Shija kuchafua hai ya hewa.

Nendeni mbadilike, nyinyi ni wakubwa kuliko klabu yeyote hapa nchini, kuanzia umri na mafanikio ya ndani, haiwezekani mukaifanya klabu yenu kama muembe wa barabarani, kila mwenye shida ya embe akajichumia tu. Nenda shija mwana wa Richard, sisi bado tunanedelea kupanda michongoma na tuna ndoto ya kuvuna miogo.