Kakolanya apigwa stop Azam

Thursday May 16 2019

 

By Thomas Ng'itu

USAJILI wa aliyekuwa kipa wa Yanga, Beno Kakolanya kutua viunga vya Azam umeanza kuota mbawa baada ya baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kupiga ‘stop’ usajili wake wakimpigia debe Metacha Mnata anayekipiga kwa mkopo Mbao.

Tangu apewe barua ya kuwa mchezaji huyu kutoka TFF,. Kakolanya amekuwa akihusishwa na klabu za Simba na Azam ambazo zimekuwa zikifanya mazungumzo ya chinichini naye. Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kigogo mmoja wa Azam (jina tunalo) amezungumza na Kakolanya na kumwambia watamalianza naye akienda na barua wa kuwa huru, lakini wenzake wakitaka arejeshwe kipa wao Metacha Mnata.

Metacha alikosa nafasi katika kikosi cha Azam na kutolewa kwa mkopo Mbao msimu uliopita, kabla ya kupelekewa Prisons ambako alikosa nafasi ya kurudishwa tena Mbao katika dirisha dogo ambako anafanya vizuri.

Kurejea kwake Mbao kulimfanya kipa huyo kung;ara katika Mashindano ya Sportpesa na kushinda tuzo ya Kipa Bora wa michuano hiyo ya SportPesa Super Cup 2019. Kung’ara kwake kulimfanya aitwe kikosi cha timu ya Taifa na kocha Emmanuel Amunike na hilo limewafanya viongozi hao wa Azam kumpotezea Kakolanya ili kumrejesha Mnata kikosini.

Mmoja wa Viongozi wa Azam alisema hawajawahi kuwa na tatizo la kipa ndio maana wanapendekeza Metacha arejeshwe badala ya kusajili kipa mpya.

“Metacha ni kipa mzuri na aliondoka hapa baada ya kukosa nafasi ya kucheza, akirejea atakuwa na wenzake Mwadini, Benedict, Abarola na mwingine wa timu ya Vijana, idadi itakamilika,” alisema huku akiomba kuhifadhiwa jina lake.a. Aliongeza harejeshwi Metacha tu, bali wachezaji wao wote waliotolewa kwa mkopo na mikataba yao ikiwa hai watarudishwa kisha ndio Kocha wao ndiye aamue vingine.

“Wachezaji wetu takribani wote ambao wametoka kwa mkopo wanafanya vizuri, kuna Cabaye nae kafanya vizuri na wengine wengi, hivyo watarejea na kocha ndiye atakayetoa maamuzi kama wapelekwe kwingine ama wakabaki Azam.”

Advertisement