Kaka wa Pogba achochea uhamisho wa dogo

Saturday August 17 2019

 

KAKA wa staa wa Manchester United, Paul Pogba, Mathias Pogba amedai lolote linaweza kutokea kuanzia sasa mpaka dirisha kubwa la uhamisho litakapofungwa kwingineko barani Ulaya na mdogo wake anasubiri ofa ya Real Madrid.

Hata hivyo, Mathias amesisitiza mdogo wake ataendelea kuitumikia Manchester United kwa moyo mmoja akitolea mfano wa staa wa PSG, Neymar ambaye anasubiri uhamisho wa kurudi Hispania huku akitakiwa na Barcelona na Real Madrid.

Man United imeendelea kusisitiza haina mpango wa kumuuza staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye mwanzoni mwa dirisha lililofungwa akiwa nchini Japan alidai kwamba anataka kupata changamoto mpya nje ya Manchester United.

Staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa moja kati ya ndoto zake ni kucheza katika klabu ya Real Madrid akipigiwa upatu na Kocha Zinedine Zidane ambaye anamtaka staa huyo kwa nguvu zote.

Man United inaweka ngumu kumtoa Pogba kwa sababu kwa sasa haitaweza kusajili mchezaji yeyote wa kuziba pengo lake baada ya dirisha la Uingereza kufungwa.

Advertisement