Kahawa imekuwa chungu kwa Zahera

Muktasari:

Nadhani hata ubingwa wa msimu uliopita wa Simba haukuwauma kwa sababu wengi waliamini kuwa walikuwa kwenye kipindi cha mpito na waliacha mdomo wa Haji Manara ushike hatamu kwasababu hawakuwa na majibu zaidi ya Zahera aliyekuwa “Celebrity” tayari.

Kahawa imekuwa chungu kwa Zahera. Maisha yana vingi vya kutupatia ndani yake kukiwa na shida na raha. Ni lazima uwe upande mmoja, hakuna katikati. Hili la kwanza litakupatia amani ya moyo huku hili jingine likikupatia huzuni kwelikweli.

Wakati tukiwa tunawaza masuala ya maendeleo ya kifedha, kuna kundi Tanzania lipo kwenye hali hii ya pili, hali iliyoambatana na shida, linaitwa Yanga. Yanga waliishi katika ulimwengu wa matumaini msimu uliopita, ambapo kila walipoona jitihada za Ibrahim Ajibu, jasho la Kelvin Yondani, ubora Feisal Salum na umaridadi wa Makambo waliamini kuwa nchi ya ahadi haiko mbali.

Waliishi katika imani kuwa Mwinyi Zahera alikuwa anawasogeza mahala salama na angeweza kuwa mhimili wao wakati wanataka kuanguka ama kuwapa hifadhi kipindi hicho ambacho walikumbwa na njaa huku majirani zao wakisherehekea mavuno ya Mo Dewji.

Nadhani hata ubingwa wa msimu uliopita wa Simba haukuwauma kwa sababu wengi waliamini kuwa walikuwa kwenye kipindi cha mpito na waliacha mdomo wa Haji Manara ushike hatamu kwasababu hawakuwa na majibu zaidi ya Zahera aliyekuwa “Celebrity” tayari.

Walioumbwa kwa roho za wasiwasi walianza kuona mwanga ukififia na giza likisogea pale alipoondoka Makambo, mshambuliaji bora ambaye ndo kwanza alikuwa anaanza kusimika mkuki wake mlangoni.

Wenye roho ngumu waliamini wanaye kocha mbaye ameaminika mpaka timu ya Taifa ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, kocha ambaye anatoa maelekezo kwa Mputu, Mulumbu, Bolasie, Masuaku na Bakambu hivyo alijua nini anafanya na kipi ambacho Yanga inahitaji.

Timu pia ilifanya uchaguzi wake na ikawaweka madarakani wale walioaminika. Watu mashuhuri pia wakaungana kufanya harambee ya kitaifa ambayo sio tu kwamba iliingiza Mamilioni bali pia iliwaweka wanayanga wote kwenye chungu kimoja na wakapikika vyema na kutoa chakula chenye ladha ya mshikamano.

Usajili mkubwa ukafanyika kwa safari za ndege mpaka nje ya nchi kwa akina Patrick Sibomana, Sadney Urikhob na kama haitoshi wakaupandia jahazi mpaka kuleta ndugu wa Feitoto, Abdulaziz Makame.

Wakiwa wameketi kwenye vijiwe vya kahawa, kashata zikiwa na ladha ya kipekee, washabiki waliamini kuwa sasa ulifika muda wa kuketi mbele ya televisheni kwa amani bila kufumba macho, kuvaa jezi mitaani kwa tambo na kuifungia kazi michuano ya kimataifa ambayo waliingia kwa mlango wa nyuma uliotobolewa na Simba. Kwenye masikio yao walikuwa wanasubiri kusikia Zahera akitaja idadi ya mifumo ambayo ingeweza kutokana na kikosi hiki kipya ambacho Yanga wamekileta, zaidi ya wachezaji tisa.

Rafiki wa vyombo vya habari akaanza kuchukizwa na mipango ya mechi za maandalizi, kwake haikuwa na tija. Zahera akarejea kikosini, nafasi ya Makambo akawepo Molinga ambaye ni kikundi kidogo kinachoamini kuwa atakuja kufanya makubwa.

Siku zimesogea na Yanga inaonekana kupiga hatua kumi nyuma, viongozi hawaelewi nini kinaendelea na washabiki hawaamini wanachokiona. Dunia inaenda kasi kuleta majira na usiku na mchana lakini kwao kila wikiendi haisogei vyema kwa sababu hawana uhakika wa kesho yao ndani ya uwanja. Bahati mbaya zaidi, jirani yao Kariakoo ambaye ndio mzani wanaoutumia anaonekana kuwa imara kadri siku zinavyosogea na mdomo wa Haji Manara unaendelea kutanuka zaidi.

Mwinyi Zahera lazima arudi kwenye kikokotoleo, atagundua hesabu alizozipiga hapo nyuma. Ni muhimu atizame mikanda ya video atakumbuka maneno yake, maneno yaliyoleta nguvu kwa kila shabiki aliyeketi kwenye kijiwe msimu uliopita akiamini kuwa huu ungekuwa mwaka wa mavuno.

Mashabiki wanahitaji faraja na ipo mikononi mwake, mashabiki wanahitaji tambo na zipo kwenye utashi wake. Yeye ndiye kila kitu kwa Yanga kwa sababu yeye ndiye aliyechonga barabara hii ya ambayo inaonekana ina makorongo kwa sasa na ngumu kupitika.

Akishinda atakuwa rafiki mkubwa kwa sababu tayari ni staa na anaweza kutengeneza ‘stori’ kwa vyombo vya habari. Akishindwa atakuwa adui mkubwa kwa sababu hakuna anayeweza kusadiki maneno yake tena hususani kipindi ambacho wachezaji wa zamani wa Yanga kama Athumani Idd ‘Chuji’ wanapotoka hadharani na kumwita mpiga dili.

Vijiwe wanavyoketi watu wa Yanga ni vya moto, ile kahawa iliyokuwa imebeba imani yao imekuwa chungu kupitiliza na hata kashata haziongezi ladha tena. Mpishi wao Zahera haeleweki na wengi wanaweza wasitake kumwamini. Muda bado upo lakini wa kuwafunga mdomo akina Chuji au kuwafanya waonekane wakweli.