Kagere kukiwasha

KIGALI. WAKATI Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck akiweka wazi kutowatumia baadhi ya nyota wake kwenye mechi ya watani, Yanga kwa sababu ya kuwa majeruhi, lakini straika Meddie Kagere anayedaiwa pia kuwa majeruhi yuko na timu yake ya Taifa ya Rwanda, akikimbiza mdogomdogo.

Straika huyo ana uwezekano mkubwa wa kuikosa Yanga wikiendi hii, lakini anaweza kukiwasha akiwa na Amavubi kwa mujibu wa kigogo mmoja wa benchi la ufundi.

Kagere amekosa mechi kadhaa za Ligi Kuu Bara akidaiwa ni majeruhi, lakini alijumuishwa katika kikosi cha Amavubi inayojiandaa na mechi ya kufuzu michuano Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Cape Verde wiki ijayo.

Mechi hiyo inachezwa Novemba 11, mwaka huu jijini Kigali ambapo Kagere alikuwa mchezaji wa kwanza kuripoti kambini na kuanza mazoezi akiwa chini ya jopo la madaktari.

Kagere anafanyishwa mazoezi ya pekee yake tangu alipojiunga na kikosi hicho Jumatano na ameanza pia kucheza mpira kumuweka fiti kabla ya kuikabili Cape Verde huku ikielezwa kuwa Simba ilimpa ruhusa ikimtaka akatulie ajiuguze kwanza.

Kagere aliondoka jijini Dar es Salaam wiki iliyopita huku taarifa za ndani zikieleza kuwa, aliuomba uongozi wake kumpa ruhusa ya kuja kutibiwa zaidi nyumbani chini ya uangalizi wa Daktari wa Amavubi.

Mpaka anakwenda kujiunga na timu hiyo, Kagere alikuwa amekosa mechi tatu dhidi ya Prisons, Ruvu Shooting ambazo walipoteza zote ambapo kila moja walifungwa bao 1-0 pamoja na Mwadui FC walioibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Hata hivyo, Kagere ambaye ana mabao manne ameonekana kuwa katika wakati mgumu kwani, mara kadhaa amekuwa akitokea benchi ambapo mara nyingi Sven hupenda kumtumia John Bocco mwenye mabao matatu sawa na Chris Mugalu.