Kagere hesabu zipo Kongo

Muktasari:

  • Mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere alisajiliwa na kikosi hicho mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu Bara akitokea Gor Mahia ya Kenya. Tangu asajiliwe na kufanya kazi pamoja na Kocha Mkuu Patrick Aussems amekuwa tegemeo na kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo.

STRAIKA Meddie Kagere amefichua kuwa, mechi ya JS Saoura imeisha na sasa yeye na wenzake lazima waelekeze nguvu kwenye mchezo wao wa wikiendi hii dhidi ya AS Vita ya DR Congo ili kuendelea kuwapa raha mashabiki.

Kagere aliyefunga mabao mawili na kuipa ushindi wa mabao 3-0 timu yake, alisema kuwafunga JSS kwake sio ishu kwani anarekodi ya kuwanyamazisha, lakini hesabu zake zipo kwenye mechi hiyo mjini Kinshasa.

“Tuna mechi dhidi ya Vita tunatakiwa tushinde, hii ndio mechi ngumu kwa sasa hatupaswi kuifikiria mechi ya JSS, wale ugenini wanacheza mpira wa kawaida sana ndio maana tumewanyuka, lakini kazi ipo mbele yetu dhidi ya AS Vita,” alisema na kuongeza kuwa wanakwenda ugenini na hawapaswi kufanya makosa ili wavune alama tatu za kuwaimarisha kileleni kwenye kundi lao.

Kuhusu kasi ya kufunga, alisema amekuja Simba kufanya hivyo na atazidi kufunga anapopata nafasi ili kuiwezesha timu hiyo kufika mbali zaidi.

“Napenda kufanya kitu cha tofauti kila siku, hiyo ndio falsafa ya maisha yangu sehemu yoyote ile, hivyo nikifunga leo nataka nifunge kesho na kesho kutwa na ndivyo nilivyo.”