Kagere aibua vita mpya Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Dilunga alisema vita yake ni dhidi ya wachezaji wa kigeni, akisisitiza kiatu cha dhahabu kibaki kwa wazawa na kuwashauri Salum Aiyee (Mwadui FC mabao 10) na Dikson Ambundo (Alliance mabao 8) kukaza buti ili kutunze heshima ya rekodi aliyoacha Simon Msuva mwaka 2017 ya kuwa mfungaji bora kwa mabao 14.

STRAIKA wa Ruvu Shooting, Said Dilunga amesema kasi ya Meddie Kagere ni kubwa ambayo italeta changamoto ya kinyang’anyiro cha nani zaidi wa kuzifumania nyavu.

Dilunga anamiliki mabao 10 sawa na ya Eliud Ambokile anayecheza soka la kulipwa Afrika Kusini, alisema Kagere amefunga mara mbili mfululizo dhidi ya Mwadui FC na kufikisha mabao nane ya ligi kuu na ligi ya mabingwa Afrika ambapo alifunga dhidi ya Al Ahly.

“Tabia ya straika akiwa anafunga mfululizo anakuwa na mzuka wa kufanya vizuri zaidi ndicho ninachokiona kwa Kagere sasa.

“Jamaa alifunga dhidi ya Mwadui FC amekuja kufunga na Al Ahly mechi yao ya kimataifa akiendelea hivyo kutakuwa na ushindani wa nani kinara wa mabao kwa sisi ambao tuna mabao mengi,” alisema.

Dilunga alisema vita yake ni dhidi ya wachezaji wa kigeni, akisisitiza kiatu cha dhahabu kibaki kwa wazawa na kuwashauri Salum Aiyee (Mwadui FC mabao 10) na Dikson Ambundo (Alliance mabao 8) kukaza buti ili kutunze heshima ya rekodi aliyoacha Simon Msuva mwaka 2017 ya kuwa mfungaji bora kwa mabao 14.

“Inawezekana wazawa kuchukua kiatu cha ufungaji bora huku tukijifunza kwa nini wageni wana kasi, mfano tusichukulie pia kuhusu Kagere ambaye anafunga kwa mfululizo na sisi tunatakiwa kukaza buti tutafika,” alisema.