Kagere: Niyonzima madini, msimchukulie poa!

Sunday September 9 2018

 

By OLIPA ASSA

PAMOJA na Haruna Niyonzima kukosa nafasi ndani ya kikosi cha Simba, unaambiwa huko kwao Rwanda ni habari ya mjini na ndiye atakayevaa beji leo Jumapili wakati Amavubi ikivaana na Ivory Coast katika mechi ya kuwania fainali za Afcon 2019 kule Cameroon.

Unajua aliyeyasema hayo? Wala sio mwingine ila ni straika matata wa Simba, Meddie Kagere alifichua Niyonzima alivyo mtamu tofauti na jinsi mashabiki wa soka nchini wanavyomchukulia na kumuona wa kawaida sana.

Kagere anayecheza na Niyonzima katika timu hiyo ya taifa ya Rwanda, alisema kiungo huyo bado ana madini mguuni kwake na kwamba kuna changamoto alizokutanazo ndani ya Simba na kumpotezea yale makali aliyokuwa nayo Yanga.

Straika huyo alielezea namna ambavyo Niyonzima alikuwa akifanya maajabu kwenye mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao huo akiwashangaza baadhi ya wachezaji na kuona anakosaje namba ndani ya Simba kwa kiwango alichoonyesha.

“Hapa namzungumzia nahodha wa timu ya taifa na sio klabu yangu ya Simba, huyu Niyonzima wa Rwanda ni hatari, anafanya vitu vinavyopendwa na wenzake pamoja na benchi la ufundi kwa hakika bado ataendelea kufanya maajabu katika soka.

“Naamini atafanya vizuri katika mechi yetu ya kesho (leo), ndipo ninachokiongea kitathibitika uwanjani atakapokuwa kazini kwani soka linachezwa uwanjani na sio sirini kwamba watakuwa hawaoni,”alisema.

Mbali na hilo Kagere alisema anafurahi kucheza pamoja na Niyonzima kwenye kikosi chao cha taifa, kwa madai wanaendelea kuzoeana na kila mmoja kutambua uwezo wa mwenzake.

“Kwanza nampa heshima ya unahodha, lakini pia najisikia vizuri kucheza naye, naamini tutafanya kitu cha tofauti kwa nchi yetu,” alisema Kagere.

Niyonzima alijiunga na Simba msimu wa 2017/18 akitokea Yanga ambako alioanza kuwatumikia mwaka 2011 akitokea APR ya Rwanda, wakati huo alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu hata kuitwa ‘Fabregas’.

Advertisement