Kagere, Mugalu washtua

HII huenda ni taarifa mbaya kwa mashabiki wa Simba, lakini ni nzuri kwa wenzao wa Yanga baada ya kufichua kuwa, washambuliaji hatari wa Simba, Meddie Kagere na Chriss Mugalu sambamba na kiungo, Gerson Fraga huenda wakalikosa pambano la derby kati yao na Yanga litakalopigwa Jumamosi hii.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck ametamba hata bila nyota hao bado ana uhakika wa kuinyoosha Yanga kwenye pambano hilo lililoahirishwa awali kutoka Oktoba 18 nadi Novemba 7.

Fraga na Kagere wote wanasumbuliwa na maumivu ya goti na Mugalu akiuguza maumivu ya misuli na Kocha Sven amefichua kuwa habari mbaya kwao kwa kuwakosa nyota hao kwa mechi hiyo ya watani.

Awali Kagere alishakosa mechi tatu dhidi ya Tanzania Prisons, Ruvu Shooting na Mwadui, lakini Sven ameweka wazi kwamba nyota huyo atendelea kukosekana katika kikosi chake.

“Ni habari mbaya lakini ukweli ni kwamba (Kagere) ataendelea kukosekana kwa wiki mbili au tatu katika kikosi chetu, sio yeye tu hata Chris (Mugalu) bado kuna hatihati,” alisema Sven na kuongeza;

“Kwa Fraga ni habari mbaya zaidi kwani atakosekana mpaka mwisho wa msimu na hii ni baada ya kugundua tatizo lake hasa ni nini.”

Hata hivyo Sven ametamba licha ya kukosekana kwa Kagere, bado hana wasiwasi wowote kwani katika kikosi chake kila mchezaji anafunga na kuisaidia timu na hata siku ya Debry anahakika ya kushinda.

“Simba kila mchezaji anafunga, Bocco anafunga, Dilunga amefunga, Ajibu amefunga na hili ndio jambo zuri kila mchezaji akiwa anafanya hivi,” alisema Sven na kuongeza;

“Unajua timu kubwa inahitaji presha na sasa tuna tofauti ya pointi sita tu na msimu uliopita wakati tunacheza nao tukafunga 1-0 tulikuwa na tofauti wa pointi nane, tunahitaji presha ili tusijisahau kwa sababu tunataka turudi kileleni.”

Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema majeraha ambayo aliyapata Kagere na Fraga ambaye aliumia goti ni wachezaji wachache mno ambao hupona kwa haraka.

Gembe alisema Kagere anaweza kurejea haraka kutokana na jeraha lake la mguu kuendelea vizuri lakini Fraga inabidi apate matibabu zaidi ya goti na baada ya hapo apate muda wa kutosha kupumzika.

“Wote wawili kama ilivyoeleza kocha ni ngumu kuwepo katika mechi na Yanga ila kubwa ambalo linafanyika wakati huu ni kupewa uangalizi na matibabu ya kila wakati ili ndani ya muda sahihi waweze kupona na kurejea katika majukumu yao,” alisema Gembe.

Simba ilikutana na Yanga mara ya mwisho kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), Fraga alianza katika kikosi cha kwanza na alifunga bao la kwanza wakati Clatous Chama, Luis Misquisson na Mzamiru Yassin huku lile la kufutia machozi la Yanga likifungwa na Fei Toto.