Kagere, Molinga wameshikwa

Wednesday July 8 2020

 

By YOHANA CHALLE

WAKATI fukuto la mtanange la watani wa jadi likizidi kupamba moto huko mtaani, huku kila mmoja akisifia kikosi chao kuelekea mchezo wa Jumapili katika kipute cha Azam Sports Federation (ASFC), bado washambuliaji wa timu hizo wana mlima mrefu wa kuupanda.

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ndiye kinara wa kucheka na nyavu Ligi Kuu akiwa amefunga mabao 19 na ndiye mfungaji bora msimu uliopita alipocheka na nyavu mara 23 na anategemewa Jumapili.

Upande wa Yanga, David Molinga mwenye mabao 10 ndio kinara wa kucheka na nyavu na tayari kocha mkuu, Luc Eymael amempa kazi maalumu ili aweze kumpa nafasi kwenye mchezo huo.

Hata hivyo, kwenye Kombe la ASFC washambuliaji hao hawafurukuti kwani huku kuna vidume vinavyotamba kwa mabao. Kinara wa kucheka na nyavu kwenye kombe la ASFC ni Yassin Omary mwenye mabao tisa kutoka Timu ya Pamana FC ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ambayo iliishia hatua ya 16 baada ya kutolewa na Sahare All Stars kwa mabao 5-2.

Alifunga mabao yake katika mchezo dhidi ya Magereza FC akipiga hat trick walipoibuka na ushindi wa mbao 4-1, akatupia nne kwenye ushindi wa mabao 6-4 mbele ya Timberland FC na akiatupia bao moja moja dhidi ya Eagles FC na Area C walipoichapa 2-1.

“Malengo yangu ni kucheza hadi kufika ‘national team’, japo sasa hivi ni mwajiliwa wa serikali (mwalimu) lakini bado nina hamu ya kutimiza malengo yangu kwenye soka. Omary alikuwa kwenye kikosi cha Mgambo Shooting kilichopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2013/14 na mchezo wake wa kwanza kucheza Ligi kuu ulikuwa dhidi ya Yanga na kupoteza kwa kuchapwa 3-0.

Advertisement

Wachezaji wengine wanaofuata kwa mabao ni Ibrahim Ramadhan (Panama FC) mwenye mabao nane, William Mgayai (Polisi Rangers) Kessy Nassor (Jeshi Warriors) wote wakiwa na mabao manne.

Advertisement