Kagere, Chama wapewa siku mbili kutua Dar

Muktasari:

Miongoni mwao ni kocha mkuu Sven Vandenbroeck ambaye yupo Ubelgiji, kocha wa viungo Adel Zrane ambaye ni raia wa Tunisia na pia wachezaji waliosafiri kwenda kwao Sharaf Shiboub (Sudan), Clatous Chama (Zambia) na Meddie Kagere (Rwanda

Dar es Salaam. Wakati nyota wa timu nyingine wakiendelea na likizo za mapumziko, wachezaji na benchi la ufundi la Simba wametakiwa kurejea kazini kabla ya Jumanne, saa 6.00 mchana vinginevyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Agizo hilo limetolewa na mtendaji mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa kupitia taarifa yake kwenda kwa maofisa wa benchi la ufundi, wachezaji na watumishi wa Simba ambao kwa sasa wapo mapumzikoni ikiwa ni hatua ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
“Hii inafuatia memo iliyotolewa Machi 18 na tafadhali pokea muendelezo wa taarifa hiyo kwamba, wachezaji wote wa kikosi cha wakubwa wanatakiwa kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata mrejesho wa kuanza maandalizi kwa ajili ya ligi. Zoezi hilo litafanyika kambini Mbweni, Machi 31,2020 saa 6.00 mchana.
Wachezaji na wafanyakazi wote wa kigeni nao wanatakiwa kuripoti nchini Machi 31, 2020 ili kuendelea na karantini kama ilivyoelezwa na mamlaka za afya hapa Tanzania,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:
“Benchi la ufundi, wachezaji na wafanyakazi wanakumbushwa kufuata na kutii mikataba ya ajira na kutekeleza maelekezo ambayo watapewa na uongozi.”

Agizo hilo huenda likawaweka katika wakati mgumu zaidi wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi wa kigeni ambao baadhi wapo katika nchi zao kwa mapumziko hayo na wanaweza kutofika kwa wakati uliopangwa kutokana na changamoto ya usafiri wa anga iliyopo katika nchi mbalimbali duniani kutokana na tishio la virusi hivyo.
Miongoni mwao ni kocha mkuu Sven Vandenbroeck ambaye yupo Ubelgiji, kocha wa viungo Adel Zrane ambaye ni raia wa Tunisia na pia wachezaji waliosafiri kwenda kwao Sharaf Shiboub (Sudan), Clatous Chama (Zambia) na Meddie Kagere (Rwanda).
Katika hatua nyingine, meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema hajapokea taarifa za majeruhi kwa mchezaji yeyote katika kipindi hiki ambacho wako mapumzikoni.