Kagere, Chama wapewa rungu Simba

Muktasari:

Katika mazoezi ya juzi Jumanne Bocco alikosekana, huku Kagere na Chama waliwekwa pembeni na Kocha Aussems alisema aliamua kuwapumzisha wachezaji hao ili kuepukana na tatizo la majeraha baada ya kumkosa mshambuliaji wake John Bocco.

MSAFARA wa UD Songo ya Msumbiji unatarajiwa kutua nchini kesho Ijumaa, kalini wasichokijua ni kwamba wamewaandalia maafa makubwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam baada Meddie Kagege na Clatous Chama kukabidhiwa rungu Msimbazi.

Nyota hao ambao waliifungia Simba jumla ya mabao 11 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita wakati timu yao ikifika robo fainali, wamekabidhiwa rungu hilo na Kocha Patrick Aussems ili kuwamaliza wapinzani wao hao kutoka Msumbiji.

Ipo hivi. Simba wanaendelea kujifua kwenye mazoezi makali kwenye viwanja vya Gymkhana na katika kutafuta dawa ya kupata ushindi mapema mbele ya UD Songo katika mechi ya marudiano ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, Kocha Aussems ameamua kuwapa majukumu mazito Kagere na Chama akishirikiana na Francis Kahata.

Hii ni baada ya safu yake ya ushambuliaji kubainika itakosa huduma za nahodha John Bocco na Ibrahim Ajibu ambao ni majeruhi na kocha Aussems alisema;

“Bocco atakosekana sio kwa siku moja au mbili, anaweza akakosekana kwa wiki kadhaa na tayari nimeanza kuandaa utaratibu mwingine kuhakikisha tunapata matokeo katika mchezo huu licha ya ugumu uliopo wa kubaki na mshambuliaji mmoja.”

Katika mazoezi ya juzi Jumanne Bocco alikosekana, huku Kagere na Chama waliwekwa pembeni na Kocha Aussems alisema aliamua kuwapumzisha wachezaji hao ili kuepukana na tatizo la majeraha baada ya kumkosa mshambuliaji wake John Bocco.

“Unajua mpaka hivi sasa sina mshambuliaji mwingine zaidi ya Kagere, washambuliaji wangu wote wameumia miguu na siwezi kuwalazimisha kucheza, lazima niwe na uoga na Chama pamoja na Kagere, nitakuwa nawapa mazoezi madogo madogo kuelekea katika mchezo huo kwani tunataka matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wetu UD Songo.”

AJIBU, MANULA WAREJEA

Katika hatua nyingine Ibrahim Ajibu na Aishi Manula wamerejea katika kikosi cha Simba na kuanza mazoezi mepesi na kuongeza mzuka kikosini mwa vijana hao wa Msimbazi.

Manula na Ajibu walipata majeraha wakiwa na kikosi cha timu ya Taifa, hali hiyo iliwafanya wakosekane katika klabu yao ya Simba katika michezo kadhaa ya kirafiki pamoja na Ngao ya Jamii na ule wa kwanza dhidi ya Ud Songo.

Lakini Jumanne wachezaji hao walianza mazoezi na wenzao, Ajibu alionekana kuanza mdogo mdogo huku Manula akipiga tizi kali na makipa wenzake Beno Kakolanya na Ally Salum.

TIZI LILIVYOKUWA

Katika mazoezi hayo kocha Aussems alikuwa akitumia njia ya kupiga mipira ya krosi ili kuweza kupata mabao.

Aussems alikata uwanja na kupanga timu mbili, Kakolanya Beno, Yusuph Mlipili, Kennedy Juma, Santos Da Silva, Haruna Shamte, Hassan Dilunga na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ huku timu nyingine akiwapanga Aishi Manula/ Ally Salum, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Gadiel Michael, Francis Kahata, Sharif Shiboub, Gerson Fraga, Mzamiru Yassin, Shomari Kapombe na Deo Kanda.

Huku kitu kikubwa kilikuwa kikiangaliwa ni namna ambavyo mabeki wa pembeni pamoja na mawinga walikuwa wanaweza kupiga krosi na kuzalisha mabao.

Aussems alisema anataka mabao katika mchezo huo ili kuhakikisha anasonga mbele katika hatua inayofuata.

“Mazoezi ambayo tunayafanya hivi sasa ni kwa ajili ya kufunga zaidi, tunahitaji ushindi na sio kitu kingine chochote kile,” alisema.