Kagere? Chama ndiye ainyimaye raha Yanga

KAMA ulikuwa unadhani Meddie Kagere ndiye mchezaji anayewanyima raha Yanga, basi umekosea kwani unaambiwa hakuna mchezaji anayewatia tumbo joto Wanayanga kama Mzambia Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’.

Siri hiyo imefichuliwa juzi na mmoja wa viongozi wa matawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, Shaaban Omary ‘Uda’ aliyedai Chama ndiye anakuwa anawakosesha raha wakibaini kuwa amepangwa dhidi ya kikosi chao.

Uda, ambaye ni makamu mwenyekiti wa matawi hayo ya Yanga, alisema kwenye mguu wa Chama kuna ‘madini’ ambayo si rahisi kuonekana kama anavyofunga Kagere na kuwafanya mashabiki wake kushangilia na kuwanyima amani wapinzani wake.

“Chama ndiye mwiba kila Simba ikicheza na Yanga, kwanza jamaa ni fundi ana akili nyingi kuliko nguvu, anaweza asiwe anaonekana kirahisi kutokana na kubanwa,” alisema.

“Mara nyingi wanakuwa wanaonekana washambuliaji kwa sababu raha ya mashabiki ni kuona timu inafunga, hivyo wanakuwa wanamuangalia mmoja bila kuangalia timu nzima nani kafanya nini.”

Alisema uzuri wa Kagere unaonekana John Bocco akiwemo ndani, lakini anapokosekana inakuwa vigumu yeye kufurukuta na kuonyesha maajabu.

“Chama namfananisha na jinsi alivyokuwa anatusumbua Zamoyoni Mogella zamani, licha ya kwamba hakuwahi kutufunga ila alikuwa mwiba kutokana na usumbufu wake,” alisema Uda anayeongoza matawi ya Wanajangwani..