Kagere, Balama mambo yao safi

Muktasari:

Mechi alizomaliza dakika 90 ni dhidi ya JKT Tanzania katika duru zote mbili kama ilivyo kwa Mtibwa Sugar na Lipuli. Michezo mingine aliyotumika kwa muda wote uwanjani ni zile dhidi ya Biashara United, Azam, Singida United, Mwadui, Mbeya City, Tanzania Prisons, KMC, Alliance, Namungo, Coastal Union na Kagera Sugar.

ACHANA na rekodi ya kupiga mabao anayotamba nayo straika wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere. Yeye ndiye amecheza mechi nyingi zaidi ndani ya kikosi hicho, huku kule Yanga akitamba Mapinduzi Balama ‘Kipenseli’.

Mfungaji bora huyo wa msimu uliopita akipachika 23, ndiye kinara wa mabao kwa sasa akikwamisha wavuni 13, huku akifuatiwa na Reliants Lusajo wa Namungo na Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar ambaye kila mmoja amefunga tisa.

Kagere amedhihirisha hakamatiki ndani ya Simba baada ya kuongoza kwa kucheza idadi nyingi ya mechi za Ligi Kuu Bara kuliko mchezaji mwingine.

Kati ya mechi 23 ilizocheza Simba, Kagere amekosa mbili tu dhidi ya Ndanda na Mbao, huku akikinukisha katika mechi 17 kwa dakika zote 90 na nne akipishana na watu. Rekodi zinaonyesha straika huyo ametumika zaidi ya dakika 1,700.

Mechi alizomaliza dakika 90 ni dhidi ya JKT Tanzania katika duru zote mbili kama ilivyo kwa Mtibwa Sugar na Lipuli. Michezo mingine aliyotumika kwa muda wote uwanjani ni zile dhidi ya Biashara United, Azam, Singida United, Mwadui, Mbeya City, Tanzania Prisons, KMC, Alliance, Namungo, Coastal Union na Kagera Sugar.

Mechi alizotoka na kuingia ni dhidi ya Kagera Sugar ya duru la kwanza alimpisha Mbrazili Wilker Da Silva, ile ya Ruvu Shooting akipokewa na Ibrahim Ajibu, dhidi ya Yanga akimpa nafasi nahodha wake, John Bocco na Polisi Tanzania aliyoiingia kumpokea Hassan Dilunga.

Akizungumza na Mwanaspoti juu ya kuwa kinara wa kutumika dakika nyingi ndani ya Simba, Kagere alisema: “Kufanya kwangu vizuri na kuaminiwa na makocha tofauti ni kwa sababu najituma, nidhamu na ushirikiano na wenzangu.”

Kipa Aishi Manula ndiye anayemfuata Kagere kwa kucheza mechi 17 kati ya 23, akizikosa sita ambazo ni dhidi ya Lipuli FC, Mbao FC, Alliance FC, Namungo FC, Coastal Union na Polisi Tanzania ambazo zilidakwa na Beno Kakolanya. Ikiwa na maana ametumika pia kwa dakika 1,530.

Manula analingana na Muivory Coast Pascal Wawa aliyecheza dhidi ya Kagera Sugar, Biashara United, Azam FC, Singida United, Mbeya City, Tanzania Prisons, Ruvu Shooting, Lipuli FC, KMC, Yanga, Mbao FC, Alliance FC, Namungo FC, JKT Ruvu, Mtibwa Sugar, Lipuli FC na Kagera Sugar.

Akikosa dhidi ya JKT Tanzania, Mtibwa Sugar, Ndanda FC, Polisi Tanzania pamoja na Coastal Union huku Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akicheza 16 kati ya 23.

Kinara huyo akishirikiana na wenzake wameibeba timu yao ya Simba kwa kukaa kileleni kwa muda mrefu kwa kukusanya jumla ya pointi 59 katika mechi 23, wakifuatiwa na Azam yenye alama 45 na Namungo na Yanga zikifuata kila moja ikikusanya pointi 40, japo Yanga ina michezo mwili mkononi.

MAPINDUZI NAYE

Wakati Kagere ameng’ara kikosini mwake, huku Yanga anayetamba ni Mapinduzi Balama aliyekosa michezo mitatu tu.

Mapinduzi aliyesajiliwa na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Alliance FC, amekosa kucheza mechi tatu tu za Ligi Kuu Bara kati ya 21, hakucheza dhidi ya Tanzania Prisons, Mbeya City zilizopigwa Mbeya pamoja na Alliance FC zote za mzunguko wa kwanza. Hii ina maana Kipenseli ametumika Jangwani kwa jumla ya dakika 1,530.

“Makocha wenyewe kuna kitu wanakiona kwangu, lakini kubwa ni kwa sababu najituma, nidhamu na ushirikiano mbele ya wachezaji wenzangu,” alisema Mapinduzi.

Meneja wa kikosi cha Yanga, Abeid Mziba, aliweka wazi kuwa katika rekodi zake, Balama ndiye anaongoza kucheza michezo mingi.