Kagera Sugar yajipa matumaini kuivaa Prisons

Mwanza. Iko hivi, Kagera Sugar ilipata pointi moja dhidi ya Ndanda ikiwa ugenini juzi,lakini Benchi la ufundi la timu hiyo limefurahia alama hiyo na sasa wanajipanga kuwakabili Prisons.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Kagera Sugar walianza kuandika bao kupitia kwa Abdalah Mguhi dakika 27, kisha Mrisho Ngassa kuisaswazishia timu yake  dakika ya 33.

Kwa matokeo hayo yanaifanya Kagera Sugar kufikisha pointi 22 na kukaa nafasi ya 13, huku Ndanda wakiwa na alama 23 katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Ally Jangalu alisema kuwa baada ya kuambulia pointi moja, sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo ujao dhidi ya Prison kuhakikisha wanashinda.

Alisema kuwa mkakati wao ni kupambana mechi zilizobaki kushinda yote ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu na kusema kuwa timu imebadilika tofauti na walivyoanza mashindano.

“Tulianza vibaya ligi, lakini kadri tunavyosonga mbele timu inabadilika, kwa ujumla tunashukuru kwa pointi moja hii na sasa tunaelekeza nguvu kwa mchezo ujao dhidi ya Prisons,” alisema Jangalu.

Kocha huyo alisisitiza kuwa Kagera Sugar haiwezi kushuka daraja kirahisi, kwani kipindi ligi imesimama mapungufu yote yalifanyiwa kazi na sasa ni mwendo wa kusaka pointi tu.