Kagera, Polisi yazitega Simba, Yanga

Muktasari:

Hata hivyo, ushindi unaonekana hautakuwa jambo rahisi kwa Yanga kwani inakutana na Polisi Tanzania ambayo imekuwa ikionyesha kiwango bora katika mechi za hivi karibuni lakini pia ikiwa na hali nzuri kisaikolojia kutokana na kumbukumbu nzuri ya utemi iliyonayo dhidi ya Yanga.

Dar es Salaam. Kumbukumbu ya unyonge dhidi ya Kagera Sugar na Polisi Tanzania ni jambo linaloweza kukoleza ugumu wa mechi za leo za Simba na Yanga dhidi ya timu hizo katika viwanja tofauti.

Wakati vigogo hivyo viwili vya soka vikiwa na shauku ya kupata pointi tatu muhimu katika mechi za leo, hamu ya kulipa kisasi dhidi ya Polisi Tanzania na Kagera ambazo zimekuwa timu sumbufu dhidi yao inaweza kufanya mechi hizo kuwa na ushindani wa hali ya juu.

Yanga inayoshika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, baada ya kutoka sare mbili mfululizo dhidi ya Mbeya City na Prisons, itakuwa na mtihani mgumu mbele ya Polisi Tanzania mchezo utakaochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Ikiwa imezidiwa kwa pointi 17 na Simba inayoongoza msimamo wa ligi, Yanga inahitaji ushindi tu ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Hata hivyo, ushindi unaonekana hautakuwa jambo rahisi kwa Yanga kwani inakutana na Polisi Tanzania ambayo imekuwa ikionyesha kiwango bora katika mechi za hivi karibuni lakini pia ikiwa na hali nzuri kisaikolojia kutokana na kumbukumbu nzuri ya utemi iliyonayo dhidi ya Yanga.

Tangu ilipopanda daraja mwaka jana, Polisi haijapoteza mchezo dhidi ya Yanga kati ya mara mbili walizokutana ikipata ushindi katika mchezo wa kirafiki ambao uliwakutanisha Agosti 16, mwaka jana ambao ulichezwa ndani ya dimba la Ushirika mkoani humo, pia zilikutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru jijini na kutoka sare ya mabao 3-3.

Si tu kupata matokeo hayo bali pia Polisi ilionyesha kiwango bora katika mechi zote mbili.

Timu zote mbili zinakutana zikitegemea uimara wao katika safu za kiungo uweze kuamua mchezo huo ingawa zimekuwa na changamoto ya kupoteza nafasi za mabao.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema wanatambua ugumu wa Polisi Tanzania, kwakuwa waliwasumbua katika mchezo uliopita, lakini hawatakubali kupoteza au kuambulia pointi moja kwa mara ya pili katika mchezo huo.

“Mchezo wa kwanza tukiwa nyumbani tulikubali sare ya mabao 3-3 kama wao waliweza kutufunga kwenye uwanja wetu sisi pia tunaweza kupata matokeo ugenini mbinu na maandalizi ndio yatakayoamua matokeo na sio uwanja,” alisema Mkwasa.

Kiungo wa Polisi Tanzania, Baraka Majogoro alisema Yanga ya mzunguko huu imebadilika tofauti na ule wa kwanza lakini hilo haliwazuii kupata matokeo.

“Mechi itakuwa ngumu tofauti na mzunguko wa kwanza kwasababu Yanga wamefanya usajili katika nafasi mbalimbali, lakini tunatakiwa kupambana ili kuendelea kuwashawishi mashabiki wa Polisi kuendelea kuisapoti timu,” alisema Majogoro.

Jijini Dar es Salaam, Simba itaikaribisha Kagera katika Uwanja wa Taifa, mechi iliyopangwa kuchezwa kuanzia saa moja usiku.

Ni mechi inayoonekana itakuwa ya kisasi na hasa kwa Simba ambayo mbali na kiu ya kusaka pointi tatu, itakuwa na hamu ya kumaliza unyonge iliyonayo inapocheza uwanja wa nyumbani dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa miaka mitatu na miezi minne sawa na siku 1222, Kagera imekuwa ikiitesa Simba kila inapokutana nayo Dar es Salaam ambapo tangu ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0, Oktoba 15, 2016 hadi sasa, wamekutana mara mbili na zote Simba kapoteza.

Mei 19, 2018, Simba ilichapwa bao 1-0 katika mchezo ulioendana na sherehe za kukabidhiwa ubingwa lakini wakafungwa bao 1-0 msimu uliopita Mei 10, 2019.

Mechi baina ya timu hizo zimekuwa za ushindani na huwa ngumu kutabirika na mara zote hazijawahi kuwa na matokeo ya sare.

Uthibitisho wa hilo ni rekodi ya timu hizo katika michezo 10 iliyopita ambayo imewakutanisha katika Ligi Kuu zimekuwa hazina tofauti kubwa ya ushindi baina yao.

Simba katika idadi hiyo ya mechi wameibuka na ushindi mara sita huku Kagera wakiibuka na ushindi mara nne na michezo hiyo kumi baina yao imezalisha jumla ya mabao 23 ikiwa ni wastani wa mabao 2.3 kwa kila mechi.

Matokeo hayo na ushindani ulioonekana katika mechi 10 zilizopita baina ya timu hizo pengine ndio yamefanya hata mabenchi ya ufundi kwa timu zote mbili kuonesha hali ya kutojiamini.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema wanatambua kwamba Kagera Sugar wana kikosi kizuri, lakini hawataruhusu kutoka kinyonge uwanjani hapo.

“Tumejiandaa kuondoka na alama tatu muhimu, hatupo tayari kupoteza au kuambulia alama moja kwakuwa tunamalengo makubwa, kikubwa tunaomba mashabiki wajae uwanjani kuwapa sapoti wachezaji wetu,” alisema kocha huyo ambaye amewahi kuwa nahodha wa Simba.

Kocha wa Kagera, Mecky Maxime alisema ni mchezo wa kisasi huku akiweka wazi kuwa hawahofii kucheza ugenini kwa kuweka wazi kuwa mpira hauna nyumbani au ugenini.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu kuelekea mchezo huo kuhusiana na nani bora zaidi ya mwingine dakika 90 ndio zitakazoamua,” alisema Maxime.

Ndani ya uwanja ni mechi inayoonekana itakuwa ya kimbinu zaidi na kwa namna timu hizo ambavyo zimekuwa zikicheza, huenda eneo la katikati ya kiwanja ndilo likaamua matokeo ya mchezo huo.

Ukiondoa mechi hizo, kule Mwanza, Mbao wataialika Singida United wakati Coastal Union watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting mjini Tanga na Mbeya City itaonyeshana umwamba na Lipuli itakayochezwa Uwanja wa Samora, Iringa.

Uwanja wa Meja Isamuhyo Dar es Salaam, JKT Tanzania wataikaribisha Biashara United na kule Ruangwa, Lindi, wenyeji Namungo FC watacheza na KMC.