Kagera, Alliance wataka Kombe FA

Muktasari:

BINGWA wa Kombe la Shirikisho la Azam, ndiye huwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Siku moja baada ya kupangwa na Yanga katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, Kagera Sugar imetamba kuwa nia yao ni kutwaa taji hilo na kuiwakilisha katika Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Katika droo hiyo iliyofanyika jana, mbali na mechi hiyo, pia Simba imepangwa kucheza na Azam, Ndanda na Sahare All Stars na pia Namungo itacheza na Allince

Michezo yote hiyo kwa mujibu wa ratiba ya jana itapigwa kati ya  Juni 27 na  28 mwaka huu huku nusu fainali ikitarajiwa kuchezwa Julai.

Akizungumzia mchezo huo Kocha wa Kagera Mecky Mexime amesema, msimu huu wanalihitaji kombe hilo ili wapate nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa.

Mexime anasema mbali ya kulihitaji kombe hilo kwa sasa akili yake iko katika maandalizi ya ligi kuu baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili.

"Droo tumeisikia na kuona, ila najikita zaidi kwa ajili ya Ligi Kuu kwanza halafu mengine yatafuata hapo baadae kwa kuwa mechi iko mbali. Yanga tunawaheshimu lakini katika kulisaka hili kombe watatusamehe," alisema Mexime.

Katika hatua nyingine Kocha wa Alliance Kessy Mziray anasema, wao wanafanya maandalizi ya mechi zote kwa pamoja kwa kuwa Juni 28 sio mbali.

Anasema anaheshimu kila timu iliyofika katika hatua hii kuwa ni bora hivyo hawawezi kuibeza timu yoyote na jambo la msingi ni yeye kuiandaa timu yake.

"Mimi sikuwa na timu ila kwa muda mchache ambao nimefanikiwa kukaa na vijana hawa, naimani watafanya vizuri ila akili yangu sana inawaza kwanza kusalia ligi kuu, na hayo mengine yatafuata," alisema Mziray

Anasema Namungo ni timu nzuri na ina uwezo mkubwa hivyo mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na kila timu kuhitaji matokeo katika mchezo huo.