Kado awaambia Simba, uteja kwao mwisho leo

KIPA wa Mtibwa Sugar,Shaban Kado amesema awamu hii mastraika wa Simba,wataambulia patupu kwani vivpigo vya mechi zote mbili walivyoambulia msimu uliopita vimetosha.

Mtibwa Sugar itaikaribisha Simba leo Jumamosi katika mchezo utakaofanyika kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

 Msimu uliopita Mtibwa Sugar ilikubali kipigo cha mabao  2-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika  Septemba 13 mwaka jana na kupoteza tena kwa mabao 3-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili uliofanyika Februari 11 mwaka huu.

Kado amesema wamejipanga kuhakikisha wanafuta machungu yote ambayo waliyapata msimu ulioisha kutoka kwa Simba hivyo lazima wapambane leo na kupata ushindi.

 "Sina maana kwamba naona mchezo utakuwa mwepesi,Ila na sisi tunataka kuonyesha kwamba sio wateja wao wa kutufunga kila msimu, awamu hii ni zamu yao  kuambulia kichapo,"amesema.

Amesema amezoea kuona presha katika mechi hizo, hivyo anawaongoza chipukizi ndani ya kikosi chao kuuhukulia mchezo huo kawaida kama ilivyo mingine.

"Ni kweli madogo ambao hawana uzoefu na mechi hizo wanakuwa na presha hivyo nakuwa nawajenga kuona ni mechi ya kawaida isipokuwa wazingatie nidhamu mwanzo, mwisho,"amesema.