Kaburu arudishwa Takukuru

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu mshtakiwa wa pili katika kesi ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutakatishaji fedha, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru).

Uamuzi huo umetolewa leo asubuhi na Hakimu Mkazi Mkuu,Victoria Nongwa baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo, kumhoji mshtakiwa huyo.

Awali, wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai, aliiambia mahakama hiyo kuwa wanaomba kibali cha kuhoji mshtakiwa Nyange kwa sababu hawajapata nyaraka walizoziomba kutoka ofisi ya Aveva.

" Mheshimiwa bado hatujapata nyaraka tulizoomba  kutoka ofisi ya Aveva, hivyo tunaiomba mahakama yako, ituruhusu  tumhoji Nyange " alidai Swai na kuongeza kuwa
" Kuna nyaraka muhimu ambazo bado wamezifungia katika ofisi zao" alisema .

Baada ya Swai kutoa maelezo hayo,Hakimu Nongwa alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 25,2018, itakapotajwa.

Katika hatua nyingine, kesi hiyo imeshindwa kuendelea baada ya mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Evans Aveva kuwa mgonjwa, na hivyo kushindwa kufika mahakamani.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai alidai mshtakiwa Evans Aveva ni mgonjwa na anasumbuliwa na matatizo ya figo, hivyo ameshindwa kufika mahakamani.

"Mheshimiwa hakimu, nimepewa taarifa kutoka magereza kuwa mshtakiwa Evans Aveva ni mgonjwa anasumbuliwa na tatizo la figo na leo hajaletwa mahakamani, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" alidai Swai.

Kutokana na maelezo hayo, hakimu Nogwa aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 25, itakapotajwa.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Ildaiwa katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, 2016 Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa  Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva  kujipatia USD 300,000 wakatiakijua fedha hizo zimetokana na kughushi.