Kabunda aitaka rekodi Kagame

Friday July 12 2019

 

By Charity James

KIUNGO mshambuliaji wa KMC, Hassan Kabunda amesema wanahitaji kuweka rekodi katika mashindano ya Kombe la Kagame wanayoshiriki ukiwa ni mwaka wao wa kwanza.
KMC wamepata nafasi hiyo ya kushiriki baada ya wawakilishi wa mashindano hayo Simba na Yanga kujitoa kwa kile kilichoelezwa ni kubanwa na ratiba ya maandalizi ya Ligi Kuu pamoja na michuano ya kimataifa ambapo wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kabunda alisema kutokana na ubora wa kikosi chao ikiwa ni sambamba na uchu wa mafanikio wamejiandaa kuendeleza rekodi yao kama msimu uliopita baada ya kumaliza nafasi ya nne.
"KMC ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki ligi lakini ilimaliza ligi nafasi ya nne hivyo tunajipanga kuhakikisha hata huku pia tunapambana kuweka rekodi kwenye mashindano hayo,"
Kabunda alisema anaamini hata usajili uliofanywa na klabu yake ni mzuri na wenye ushindani mkubwa msimu ujao.
"Ni nyota wengi wapya wameingia na wengine kutoka lakini hilo haliondoi, uongozi umehakikisha unatimiza mahitaji ya timu kwenye usajili, wamefanya usajili bora utakaoendeleza mafanikio ya KMC.
"Nina imani na kila mchezaji aliyesajiliwa kikosini na kila mmoja anajua nini kimemleta KMC hivyo tutashirikiana kwa pamoja kuijenga timu ya ushindani kuanzia ndani na hata kimataifa ambapo tumepata nafasi ya kushiriki," alisema Kabunda.

Advertisement