KUMEKUCHA...Sven ahesabiwa siku Simba

MAMBO yameshatibuka huko, unaambiwa Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck kwa sasa ni kama anahesabiwa siku tu ndani ya kikosi hicho, kabla ya kufurushwa kwa kile kilichoelezwa kushindwa kuelewana na wasaidizi wake sambamba na kugombana na wachezaji kila mara.

Habari kutoka ndani ya Simba katika kuonyesha kuwa mabosi wa klabu hiyo wameanza kumchoka Sven, na kikao kilichoitishwa leo Ijumaa kumjadili kutokana na mambo mbalimbali ambayo amekuwa wakifanyiana na wasaidizi wake kiasi cha kushindwa kufanya kazi wa ufanisi.

Sven aliyesainishwa mkataba wa mwaka mmoja, inadaiwa haelewani na wenzake na juzi kati alishikana mashati na nahodha wa timu hiyo, John Bocco huku akimtimua kitemi, Ibrahim Ajibu kwa madai ya kuchelewa mazoezini licha ya kudaiwa aliomba udhuru mapema.

Mwanaspoti, lililotimba kwenye kambi ya mazoezi ya timu hiyo yaliyopo Uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju na kupenyezewa taarifa kwamba Sven hazungumzi na meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, huku pia akiwa haivi chungu kimoja na msaidizi wake, Seleiman Matola.

Taarifa hizo zilieleza mbali ya kutozungumza na Rweyemamu, pia amemzuia meneja huyo kusogelea hata eneo la kuchezea na kutojishughulisha na jambo lolote kama kupanga ratiba za timu, masuala ya kambini na hata kutoa ushauri wake katika jambo lolote lile.

Katika mazoezi ya asubuhi ya jana ambayo Sven aliwachomoa waandishi waliokwenda kuripoti akitishia kuwaitia polisi, alishuhudia meneja huyo akiwa kama mtazamaji kwa kushindwa kuwa karibu na eneo la kuchezea au kuongea lolote na Sven.

Chanzo makini ndani ya Simba kimesema kwa hali hiyo ya kushindwa kuelewana na wachezaji na wasaidizi wake, mabosi wa Simba wameitisha kikao leo pamoja na mambo mengine, watamjadili kwa nia ya kuweka mambo sawa, ikidaiwa kama sio mechi za kumalizia ubingwa basi angekuwa ameshatimuliwa mapema.

“Ukiachana na mambo hayo ikiwamo kugombana na wachezaji, lakini pia Sven hakuwa chaguo la wengi, ila Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa aliyempigia chapuo aliomba apewe ila ameonesha kuwa mjuaji wa kila jambo hata yale mambo mengine ambayo asiyoyafahamu, kwani humu ndani ya timu kwa sasa hakuna hata mtu mmoja ambaye anafurahia uwepo wake,” kilisema chanzo hicho

Katika kikao kitakachofanyika ofisi za klabu hiyo katikati ya jiji, inaelezwa mambo yanaweza kuwa machungu kwa kocha huyo, ambaye atakuwa na majukumu yake Bunju kikosi kikiendelea kujifua, kwani mabosi wa Msimbazi watakuwa wakimjadili, huku Rweyemamu akitarajiwa kuhudhuria kikao hicho.

AMTIMUA AJIBU

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu, juzi Jumatano alikutana na moto wa Sven baada ya kutimuliwa na mabegi yake wakati wa zoezi la upimaji afya kwa kuchelewa ratiba.

Inadaiwa Ajibu aliyekuwa akiishia Tabata amehamia Chanika kwa sasa kutoa udhuru ya kuchelewa akiwa njiani, taarifa zinazoelezwa zilimfikia kocha, lakini alipotua tu Mbweni akajikuta akitimuliwa kabla hata jasho la safari halijamkauka.

Inaelezwa Ajibu hakufanya jambo lolote kati ya waliyofanya wenzake siku hiyo kwani, kocha alimtaka kurudi nyumbani mpaka atakapomuita na hata jana nyota huyo hakuwapo mazoezini na wenzake.

WASIKIE HAWA

Kocha Sven alipofuatwa na mwandishi ili kuzungumza naye juu ya tuhuma hizo alikuwa mkali, lakini Rweyemamu alisema suala la kutoelewana na Sven na kufikia kumuwekea mipaka asiingie uwanjani katika eneo la kuchezea au kutoa ushauri wa aina yoyote hilo sio lake kulizungumzia.

“Nadhani jambo hili ni sahihi kwa Sven kueleza mwenyewe kuliko upande wangu, kwani ambalo nalifanya wakati huu ni kutimiza majukumu yangu ipasavyo, lakini hata suala la Ajibu pia atafutwe mwenyewe aulizwe,” alisema Rweyemamu.

Mtendaji wa Simba, Senzo alipotafutwa alisema kuhusu suala la kufukuza makocha linaweza kufanyika mara kwa mara katika kikosi hiko na wasiweze kufikia malengo yao ambayo wamejipangia katika msimu husika.

“Mwanzoni kabla ya kupoteza mechi dhidi ya JKT Tanzania kulikuwa na presha ya kumfukuza Sven, lakini baada ya kushinda mechi zilizofuata jambo hili lilimalizika na kila mtu alikuwa kimya kusherehekea ushindi,” alisema Senzo na kuongeza;

“Katika mpira kuna kipindi timu inaweza kupanda kwa maana ya kupata matokeo mazuri, lakini mambo yanapokuwa mabaya kwa kushindwa kufanya kile ambacho mnakihitaji kwa maana hiyo tutulie maamuzi sahihi ndani ya timu ndio yatafanyika.”

Kuhusu kikao cha leo Senzo hakuweza kulijibu.