KPL yatawatesa Watanzania

Monday December 31 2018

 

TIMU za wachezaji wa Kitanzania, wanaocheza soka la kulipwa Kenya zimekiona cha moto kwa kuambulia vipigo vya kufungia mwaka, 2018 huku Bandari pekee ya kiungo, Abdallah Hamis ikiambulia sare mbele ya Western Stima.

Hali ni tete kwa beki wa Kitanzania, Aman Kyata na timu yake ya Mount Kenya United ambao imekutana na kipigo cha nne mfululizo msimu huu kwenye  Ligi Kuu ya SportPesa ya Kenya ‘KPL’ .

Mount Kenya United imetandikwa ugenini na Chemelil kwa mabao 2-0, vipigo vingine vitatu ambavyo imepokea tangu kuanza kwa msimu wa 2018/19 ni kutoka kwa Sofapaka 2-1, Posta Rangers 2-1 na Tusker 3-0.

Chama la beki, Jamal Mwambeleko na kipa  Peter Manyika JR, KCB FC lenyewe limekiona cha moto kwa kutandikwa mabao 3-1 na wageni Tusker kwenye uwanja wa nyumbani.

Kipigo hicho ni cha tatu msimu huu kwa KCB FC, vipigo vingine vilikuwa mbele ya Homeboyz 1 – 0, Ulinzi Stars 3 – 1 huku ikiambulia pointi moja tu kwenye KPL  ambayo iliipata kwa kwenda sare ya bao 1-1 na Bandari.

Vipigo hivyo vimezifanya Mount Kenya United na KCB FC kuwa kwenye nafasi mbili za mwisho kwenye msimamo wa KPL.

Bandari FC anayoichezea Hamis imetoka sare ya bao 1-1 na Western Stima, timu hiyo ya kiungo wa Kitanzania, haijapoteza mchezo hata mmoja, imetoka sare mbili na kushinda mbele ya bingwa mtetezi, Gor Mahia 2-1 na Sofapaka 2-1.

Advertisement