KOCHA HONGO KAUMA: OLD IS GOLD! Amewaibua mastaa kibao wa ndondi

Wednesday April 3 2019

 

By Charles Ongadi

Nairobi. AISEE, ukubwa jiwe. Kwa baadhi ya maboksa nchini ni kama baba mlezi, kocha na ilhali kwa wengine ni mshauri mkuu katika masuala ya ndondi.

Hongo Kauma, mzaliwa wa Ahero kaunti ya Kisumu miaka 63 iliyopita, ni kocha mwenye tajriba kuu katika kufunza mchezo wa ndondi nchini ambaye kwa kipindi kirefu amefaulu katika kuwaibua maboksa mastaa nchini.

Wadadisi wengi wa mchezo wa ngumi nchini wanamfananisha na wakufunzi wa kimataifa kama Sachi Saggara kutoka nchini Cuba wakati humu nchini analinganishwa na wakufunzi wenye sifa kama Eliasi Gabriali, Eddie ‘Papa’ Mussie na Peter Moris miongoni mwa wengine wengi.

Mara baada ya kustaafu kutoka vikosi vya Majeshi na Polisi mwaka wa 1981 alikohudumu kama boksa katika uzito wa welter, Hongo Kauma ‘KK’ aliamua kujikita katika ukufunzi wa mchezo huo maarufu duniani.

KONGOWEA BOXING CLUB- 1981

Ni mwaka alioanzisha klabu ya Kongowea Boxing Club, Kisauni, Mombasa iliyobadilika na kuwa maarufu sana mkoani Pwani.

Licha ya klabu hii kutoshiriki ligi kuu, pia iliogopwa kama gonjwa la ukoma kutokana na kuwa na maboksa sugu waliotumia maarifa kuzoa ushindi jukwaani.

Sifa za klabu ya Kongowea zilivuma kama papa baharini huku maboksa wake wakiandamwa kwa lengo la kusajiliwa na klabu zilizokuwa zikishiriki Ligi Kuu miaka hiyo.

MABOKSA SABA WASAJILIWA BANDARI

Mwaka wa 1987, klabu ya Bandari (KPA) iliyokuwa ikishiriki mashindano ya Ligi Kuu wakati huo iliweza kuandika historia kwa kuwasajili maboksa saba kutoka klabu ya Kongowea chini ya Hongo Kauma.

Maboksa hao, Steve Ouma (heavy) na Solomon Adolwa (lightwelter) walioshia kuitwa katika timu ya taifa almaarufu ‘Hit Squad'.

Wengine ni Vincent Oswe(light), Amani Riziki (lightmiddle), Fred Mayabi (lightfly), Fredrick Oluoch (welter) na Mohammed Matano (bantam).

1995 - ATEULIWA KOCHA WA TIMU YA TAIFA ‘HIT SQUAD’

Baada ya kudhihirisha uwezo wake katika ukufunzi, Chama cha mchezo wa ndondi nchini kwa kauli moja ilikubaliana kwamba chanda chema huvishwa pete na kumteua kocha Hongo kamanaibu mkufunzi wa timu ya taifa.

Kocha Hongo aliandamana na na kikosi cha ‘Hit Squad' iliyoshiriki Michezo ya Bara la Afrika yaliyoandaliwa Harare nchini Zimbabwe mwaka wa 1995.

Akishirikiana na kocha mkuu Peter Mwarangu, Hongo aliweza kuingoza kikosi cha taifa iliyokuwa na maboksa kama Omar ahemd Kassongo (heavy) davis Anyim (Superheavy), Evans Ashira Oure (welter), Peter Odhiambo (middle) miongoni mwe wengine kumaliza katika nafasa ya pili katika mashindano hayo.

KK BOXING CLUB – BOMBOLULU

Mara baada ya kurudi kutoka nchini Zimbabwe, kocha Kauma aliamua kusambaza mchezo wa ndondi kote mashinani kwa kuanzisha klabu ya KK Boxing Club mwaka wa 1996 eneo la Bombolulu, Mombasa.

Baada ya kipindi kifupi kocha Hongo aliweza kumtoa boksa David Maina katika uzito wa light aliyeitwa katika kikosi cha taifa kwa majaribio.

AVUTIA WAFADHILI

Ubora wa kocha Hongo ulivutia wafadhili wengi Pwani na hata bara na wakati Fredrick Achola alipobuni klabu ya Havana Boxing Club eneo la Magongo mwaka wa 2014, aliamua kumsajili Kocha Hongo katika benchi lake la ufundi.

Kwa muda huo, mkufunzi huyu ameweza kuibadilisha klabu ya Havana kuwa miongoni mwa zile maarufu sana mkoni Pwani akifaulu kuwaibua maboksa kama Anderson Muhatia katika uzito wa lightwelter, Nicholus Macharia (middle) na chipukizi Emmanuel Muga (lightfly) ambao nyota zao zimeanza kung’ara.

MALENGO YA BAADAYE

Kocha Hongo anaazimia kubadilisha mkumbo katika ukufunzi wake kwa kuwalenga chipukizi ambao ndio msingi wa mchezo.

“Future ya boxing ni youths kwa hivyo wakati ni sasa kuweka msingi thabiti kufaulu siku zijazo,” asema kocha Hongo.

Advertisement