KMKM yaahidiwa mkwanja CAF

Muktasari:

Kocha Mkuu wa KMKM, Ame Msimu amesema tayari wameyafanyia kazi makosa ya mchezo wa kwanza, hivyo anaamini watafanya vizuri.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Seif Kombo Pandu amewaahidi mabaharia wa KMKM Dola 5,000 (zaidi ya Sh. 11 milioni) ikiwa timu hiyo itafanya vizuri kwenye mchezo wamarudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Despotivo de Agosto ya Angola.

Pandu ametoa hamasa hiyo wakati akiwaaga wachezaji na viongozi wa timu hiyo katika ofisi za shirikisho hilo, Amani mjini Unguja ambapo alisema awali aliweka ahadi ya Dola 1,000 kama timu hiyo ingeshinda katika mchezo wa awali, lakini sasa ameongeza dau ikiwa timu hiyo itapindua matokeo ugenini.

Rais huyo aliwataka wachezaji hao kusahau matokeo yaliopita ya kupoteza mchezo wa nyumbani na kuwaza ushindi ugenini kwani mpira wa miguu ni mchezo wa wazi na lolote linaweza kutokea.

Hata hivyo, Pandu amewataka wachezaji hao wakaonyeshe kama na wao wanaweza kucheza kwani hana wasiwasi kutokana na timu hiyo ilivyoonesha kiwango katika mchezo uliopita licha ya kukubali kichapo cha mabao 2-0.

Kocha Mkuu wa KMKM, Ame Msimu amesema tayari wameyafanyia kazi makosa ya mchezo wa kwanza, hivyo anaamini watafanya vizuri.

Msimu alisema licha ya kukabiliwa na mchezo huo mgumu ugenini, lakini wataenda kupambana na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili kusonga hatua nyengine ya michuano hiyo.

Hata hivyo, Msimu alisema watawakosa wachezaji wawili wa kikosi cha kwanza ambao ni majeruhi beki kisiki, Richard Jovit Jaka na Brown Bruno Costa ambapo nafasi zao zitazibwa na wachezaji wengine. Nahodha wa timu hiyo, Makame Haji Ngwali naye alisema mchezo wao wa kwanza ulikuwa mgumu kutoka na wenzao kuwa na uzoefu mkubwa kuliko wao.

Makame alisema watahakikisha wanaenda kufanya vizuri katika mchezo huo wa marudiano .