KMC yaishusha Azam kileleni

Muktasari:

Ushindi wa Kmc unawafanya wasogee mpaka nafasi ya kwanza huku wakiwa pointi tisa sawa na Azam Fc kukiwa na utofauti wa magoli tu.

 

Ushindi wa KMC wa 2-1 dhidi ya Mwadui Fc katika mchezo uliopigwa leo Jumatatu saa 8:00 mchana Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga unaifanya timu hiyo kutoka nafasi ya nne na kupanda nafasi ya kwanza.

 KMC wana pointi tisa (9) katika michezo mitatu sawa na Azam Fc huku wakitofautiana mabao ya kufungwa na kufunga, ambapo KMC wamefunga mabao nane na kuruhusu magoli mawili huku Azam wao wakifunga mabao manne na kutoruhusu bao lolote.

 Utofauti huo unawafanya KMC kuongoza ligi kutokana na kuwa na faida ya mabao sita baada ya yale nane ya kufunga na mawili ya kufungwa wakitoa yanabaki mabao sita huku Azam wakiwa na mabao manne.

 Katika mchezo huu Mwadui FC walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia Issa Shabani, lakini KMC walisawazisha kupitia mshambuliaji wao mpya Reliants Lusajo aliyefunga dakika 77 na 84.

 Ushindi huo pia unawaondoa Dodoma Jiji nafasi ya pili wakiwa na pointi saba na kushuka mpaka nafasi ya tatu kisha KMC wakipanda mpaka nafasi ya kwanza na Azam wakishika nafasi ya pili.

 Baada ya mchezo huu KMC Ijumaa, Septemba 25, 2020  watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Kaitaba, kwani timu hiyo imetoka kupoteza dhidi ya Yanga bao 1-0.