KMC yaanika kilichofanya waipeleke Yanga Mwanza

Muktasari:

KMC ilipanda Ligi Kuu Bara misimu mitatu iliyopita na katika msimu wao wa kwanza ilikata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya CAF kutoa nafasi kwa Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano ya Afrika ikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika 2019-2020.

MASHABIKI wa soka wamekuwa na maswali mengi kichwani kutokana na Bodi ya Ligi (TPLB) kutoa ratiba mpya ya Ligi Kuu Bara na kuonyesha pambano la KMC dhidi ya Yanga litapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza badala ya jijini Dar es Salaam kama ilivyokuwa inaonekana awali.
KMC ambao ni wenyeji wa mchezo huo wataikaribisha Yanga jijini humo Oktoba 25 na kuibua maswali mengi, lakini uongozi wa klabu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, imetoa ufafanuzi sababu ya kulihamisha pambano hilo Kanda ya Ziwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu ya KMC iliyotolewa na Ofisa Habari na Mahusiano wao, Christina Mwagala ni kwamba KMC imetumia ofa iliyotolewa na Bodi ya Ligi katika kikao chake cha ufunguzi wa Ligi Kuu kwa msimu huu iliyotaka kila timu kuruhusiwa kucheza michezo yake miwili ya nyumbani nje ya kituo mama, nao wakachagua mchezo wao na Yanga kwenda kupigwa Mwanza.
Uongozi huo wa KMC umesema mbali na kutumia ofa hiyo, lakini inatambua thamani ya mashabiki waliopo mikoani hapa nchini ndio maana wakaona bora wakawapelekee burudani mashabiki wa soka wa Mwanza.
"Tunafahamu kuna mashabiki wengi wa soka kila mkoa, hivyo ni nafasi kwa Wanamwanza kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili waweze kushuhudia soka safi linalochezwa na KMC dhidi ya Yanga, hivyo itakuwa ni salamu tosha kwa timu nyingine kongwe kuona ubora wa kikosi hicho," alisema Christina.
Christina alisisitiza kwa kuwasihi mashabiki hao wa Mwanza na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwa mchezo huo wa Oktoba 25, ili kuipa nguvu timu yao kupata ushindi kuendeleza rekodi yao kila wanapokutana na Yanga ndani ya Ligi Kuu ama kwenye mechi za kirafiki.
KMC walioanza ligi kwa kasi na kuongoza msimamo katika mechi tatu za awali, wameshacheza michezo mitano na kushinda mitatu na kupoteza miwili na kusaliwa na alama 9, nne pungufu ilizonazo Yanga iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo nyuma ya Simba, huku Azam FC ikiwa kileleni na pointi 15.