KMC hawana presha ya kusaka kocha mpya

Muktasari:

Huu ni msimu wa pili kwa KMC kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara  na msimu uliopita ilimaliza nafasi ya nne ikiwa na pointi 55 baada ya kucheza michezo 38 na kushinda 13, ilitoka sare michezo 16 na kupoteza tisa.

Dar es Salaam. Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta amesema timu ya KMC haina papara ya kutafuta kocha mpya kwani hivi sasa wanaendela kutafuta tatizo ndani ya timu hiyo.

Sitta amesema wanafanya mambo kwa uangalifu mkubwa ili wasije kuongeza tatizo juu ya tatizo na ndio maana bado wanachunguza kubaini tatizo ni nini linaloikabili timu hiyo kabla ya kumtafuta kocha mpya.

Mapema mwezi huu uongozi wa KMC ulimtupia virago kocha Jackson Mayanga raia wa Uganda kwa madai ya kutoridhishwa na mwenedo wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo licha ya Mayanja kutimuliwa bado KMC imeendelea kufanya vibaya kwani katika michezo mitatu ambayo kocha huyo hajakaa benchi wamepoteza yote dhidi ya Kagera Sugar kwa mabao 2-1, dhidi ya Alliance kwa mabao 2-1 na dhidi ya Mbao kwa mabao 2-0.

"Ujue kila kocha anakuja falsafa yake hivyo tunakuwa wangalifu sana katika kutafuta kocha mpa ili kuhakikisha timu inasonga mbele.

"Tunachambua kwa upana ili kujua tatizo la timu yetu hasa ni nini kwani tunaweza kubadilisha kocha kumbe tatizo lipo sehemu nyingine.

 "Matokeo haya bado hatuwezi kusema yanatuchanganya ingawa hayafurahishi, lakini bado tuna nafsi ya kufanya vizuri zaidi kwa sasa ni mapema kusema kuwa tunachanganywa na matokeo haya," alisema Sitta.