KITUO KIPYA CHA CHILUNDA MOROCCO NDO HIKI

HAINA kufeli ndio msemo ambao unaweza kutumika baada ya kuthibitika kuwa Shaaban Chilunda anaondoka Chamazi na kwenda Oujda huko nchini Morocco ambako maskani yake mapya yatakuwa kwenye uwanja wa Honneur.

Awali, Chilunda alionekana ni kama amefeli baada ya kurejea nyumbani Tanzania akitokea Hispania ambako alikuwa akiichezea CD Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania, wadau wengi walipenda kumuona akiendelea kupiga hatua.

Kumbe Chilunda alikuwa na hesabu zake tofauti kabisa kichwani mwake na ilikuwa ni suala la muda tu kuondoka tena nchini na kwenda kwenye mataifa yaliyondelea zaidi kisoka ili kupigania ndoto zake.

Licha ya kwamba mshambuliaji huyo, alisema kuwa amerejea nyumbani kujipanga, ni wachache waliokuwa wakitumaini kutokana na kile ambacho kimekuwa kikitokea kwa wachezaji walioenda nje kujaribu kwani waliporejea ilishindikana tena kutoka.

Chilunda yupo kwenye hatua za mwisho kutimkia zake kwenye maskani yake mapya Honneur kwani kila kitu kimewekwa sawa na juzi tu klabu yake ambayo alikuwa akiichezea Azam FC wamethibitisha kuwepo kwa mazungumzo na Mouloudia Oujda kuhusu mchezaji huyo.

Makala hii inakuelezea yalivyo maskani mapya ya Chilunda huko Morocco na ukubwa wa timu hiyo, mwenendo wao kwenye Ligi na mafanikio waliyonayo kwa kulinganisha na timu ambazo wanazichezea Watanzania wengine nchini humo.

MASKANI MAPYA

Honneur ni uwanja ambao Mouloudia Oujda wamekuwa wakiutumia kucheza mechi zao za nyumbani.

Dimba hilo lina uwezo wa kuingiza mashabiki wapatao 19,000 idadi hiyo ni takriban mara tatu ya mashabiki ambao wanaweza kuingia katika maskani yake ya zamani, Uwanja wa Azam Complex.

Yalipo maskani mapya ya Chilunda ni umbali wa Kilometa 715 kutoka El Jadida yalipo maskani ya Watanzania wenzake, Nickson Kibabage na Simon Msuva ambao wanaichezea Difaa Ed Jadida. Kutoka El Jadida hadi Oujda inakuchukua saa saba kufika kwa gari.

Akipazungumzia Msuva anasema, “Ni mbali kutoka kwetu lakini kwa sababu kuna wepesi wa usafiri nadhani tutakuwa tukitembeleana.”

UKUBWA WA KLABU

Mouloudia Oujda ilianzishwa mwaka 1946. Ina miaka 74 na ni miongoni mwa klabu zenye historia ya kipekee kwenye soka la Morocco.

Tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, wametwaa mataji tisa, yakiwamo manne ya Kombe la Morocco kwenye miaka ya 2003, 2007, 1964 na 2018 kwa sasa chama hilo jipya la Chilunda linaongozwa na Abdelhak Benchikha kama kocha wa kikosi hicho.

Kocha huyo aliwahi kuifundisha Difaa El Jadida lakini kwa wakati huo ilikuwa bado Msuva hajatua Morocco. Chama jipya la Chilunda linaonekana kuwa kubwa kuliko chama la Msuva na Kibabage.

Difaa El Jadida ambayo wanaichezea Msuva na Kibabage ilianzishwa 1956, tangu kuanzishwa kwa timu hiyo ambayo uwanja wao wa nyumbani unaingiza mashabiki 15,000, imetwaa mara moja ambalo lilikuwa Kombe la Mfalme, 2013.

MWENENDO WAO

Kabla ya mechi za wikiendi iliyopita ambapo ilichezwa michezo ya raundi ya 28, zimebaki raundi mbili chama jipya la Chilunda kumaliza msimu na ni kati ya timu ambazo zina nafasi ya kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Morocco tofauti na chama la Msuva.

Chama la Msuva na Kibabage, Difaa El Jadida kiwango chao kwa mwaka huu hakitofautiani na lile la Mtanzania mwingine anayecheza soka nchini humo, Maka Edward anayeichezea Moghreb Tetouan.

Mouloudia Oujda wapo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Batola Pro huku Difaa wakiwa nafasi ya saba na Moghreb iko nafasi ya nane hiyo ni kabla ya michezo ya raundi ya 28.

NYOTA KIKOSINI

Kikosi cha Mouloudia Oujda kwa asilimia kubwa kinaundwa na wazawa. Kabla ya Chilunda, kuna wachezaji watano tu wa kigeni kwenye kikosi chao ambao ni Bopunga Botuli na Nelson Munganga kutoka DR Congo.

Wengine ni Mmarekani ambaye amezaliwa nchini humo, Noah Sadaoui, Emeka Ogbugh kutoka Nigeria na Lamine Diakite wa Ivory Coast.