KITANUKA: Hapa kwenye robo fainali patamu!

HUKO kitaani kwa sasa ni tambo za watani wa jadi Simba na Yanga. Unaweza kushangaa, tambo hizo za kazi gani wakati wanaume hao walishamalizana msimu huu katika Ligi Kuu Bara.

Yanga walishanyakua pointi zao nne swafii kutoka kwa watani wao kwa kutoka sare ya 2-2 katika mechi ya mkondo wa kwanza kisha kumaliza udhia katika marudiano kwa bao murua la friikiki ya Bernard Morrison.

Kama hujui ni kwamba droo ya Kombe la FA imefanyika juzi jijini Dar es Salaam kwa mechi za robo fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Azam na inafahamika zaidi kama Azam Sports Federation Cup.

Simba na Yanga wametenganishwa katika hatua hiyo, lakini kama timu zote zitapenya hatua hiyo na kutinga nusu fainali, basi lazima kiwake. Hicho ndicho kinachowafanya mashabiki hao kuanza kutambiana mapema, kila upande wakitaka eti wakutane tena kumaliza ubishi kibabe.

Yanga wanaamini watani wao ndio watakaowapa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, wakati Simba wakiamini mechi kati yao itamaliza tambo za Wanajangwani juu ya ushindi walioupata dhidi yao katika mchezo wao wa Machi 8 na Morrison kuwalaza mapema.

Ndio, ratiba iliyorushwa mubashara na kituo cha Azam kimezipanga Simba kuvaana na watetezi Azam, huku Yanga wakipewa wabaya wao, Kagera Sugar waliowanyuka mabao 3-0 katika mechi yao ya mwisho katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Mechi nyingine zitazikutanisha Namungo dhidi ya Alliance na Sahare All Stars, timu pekee ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyosalia kwenye michuano hiyo itawaalika Ndanda kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Mwanaspoti linakudondolea kwa ufupi kazi waliyonayo Azam na namna droo hiyo ilivyovitega vigogo waliopo Tatu Bora ya Ligi Kuu Bara. Kivipi? Tiririka nayo...!

SAFARI ILIVYOKUWA

Klabu hizo nane mpaka zinafika hatua hiyo hazikufanya kazi ndogo, kwani zimepambana kutoka ndani ya timu 64 hadi kufika hapo zilipo.

Watetezi Azam wenyewe walikuwa na njia nyepesi kidogo kwani mechi zao tatu za awali ilivaana na timu za Daraja la Kwanza, ikianza na Ihefu ya Mbeya kisha kuvaana na Masela wa Manzese wanaojuana nao, Friends Rangers kisha kumalizana na watani zao, African Lyon.

Simba wao walianza kibarua dhidi ya Stand United iliyopo FDL kisha kupenya kwa mbinde mbele ya Mwadui FC na baadaye kumalizana na AFC Arusha, wakati watani zao kibarua chao kilianzia kwa Gwambina inayojiandaa kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Baada ya kupenya hapo ikavaana na Tanzania Prisons waliokuwa na rekodi ya kutopoteza mechi yoyote tangu msimu uliopita na kisha kuwazima Iringa United, wakati Kagera walipenya mbele ya KMC, Mighty Elephant na kisha Rufiji United.

Alliance wenyewe walivuka kwa kuzing’oa JKT Tanzania, Africans Sports na Transit Camp ilihali Namungo walipenya mikononi mwa Mbeya City, Biashara United na Green Warriors, wakati Ndanda nao walizing’oa Kitayosa, Dodoma FC na Cosmopolitan.

Kwa upande wa Sahare iliyoshangaza wengi, ilianza kazi kwa kuvaana na kuing’oa Panama FC, kisha ikawaduwaza mabingwa wa zamani wa Tanzania, Mtibwa Sugar kabla ya kuitoa Njombe Mji na sasa ina kibarua kingine cha kufuata kilichowahi kufanya na timu za madaraja ya chini kufika mbali kwenye michuano huyo kama Tanzania Stars, Baker Rangers ama Madini FC.

AZAM KAZI WANAYO

Licha ya Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdukarim Amin ‘Popat’ kufurahia kupangwa na Simba ili kuendelea ule ugumu wa mechi baina yao, ila ukweli Azam wanapaswa kujipanga kama kweli wanataka kufuata nyayo zilizowahi kuweka na Tanzania Stars katika michuano hiyo.

Rekodi zinaonyesha tangu kurejeshwa upya kwa michuano hiyo mwaka 2015 chini ya TFF ya Jamal Malinzi, hakuna timu iliyonyakua ubingwa wa FA na kutetea taji kwa msimu uliofuata.

Yanga na Simba, licha ya ubabe wao wote walikwama sawa na ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar waliolitema taji mbele ya Wanalambalamba ambao sasa ndio wana kibarua cha kulitetea.

Tanzania Stars ndio pekee waliwahi kuweka rekodi ya kulitetea baada ya kulitwaa mwaka 1997 na 1998 na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiundwa na maveterani ambao waliingia michuano bila ya kuwa na ndoto za kulibeba taji hilo la FA.

Mechi yao ya Simba ni kama fainali kutokana na ukweli ndio inayoangaliwa kama moja ya mechi kali zaidi kwa msimu huu ambayo hakuna anayeweza kutabiri mapema, japo Azam ni lazima watokwe jasho kama kweli wanataka kufikia ilichofanya wakongwe wa Tanzania Stars. Kwa wanaokumbuka wakati wanalitwaa taji lao la mwaka jana Azam waliifyatua Lipuli Fc kwa baop 1-0, lililowekwa kimiani na Mzambai Obrey Chirwa. Bila ya shaka hata msimu huu watakuwa na hamu ya kuona wanalibeba tena, lakini sio kazi rahisi kama hawatajipanga!

YANGA KIBOKO YAO

Licha ya kwamba Tanzania Stars iliyokuwa daraja la nne chini ya kina Idd Azan, Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kinondoni na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kile cha Wilaya ya Kinondoni (KIFA) kushikilia rekodi hiyo, Yanga nao ni noma katika FA.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania, Yanga ndio inayoshikilia rekodi ya kutwaa mara nyingi taji hilo ikifanya hivyo mara tano, tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 1967.

Walitwaa taji la kwanza michuano ilipoanza kisha kuja kuilitetea tena baada ya muda mrefu kwa michuano hiyo kutochezwa yaanui 1974 na kurudia tena 1999, 2001 na msimu wa 2015-2016 iliporudi upya kwa mfumo wa sasa baada ya kusimama tangu ilipochezwa mara ya mwisho 2002.

Timu nyingine zilizobeba taji hilo mara nyingi ni Simba, Tanzania Stars na Mtibwa Sugar zilizotwaa mara mbili mbili kila , huku Sigara, Majimaji na JKT Tanzania (zamani JKT Ruvu) nao wakilitwaa mara moja moja katika misimu tofauti ya kufanyika kwake.

Hii ndio mechi itakayoamua hatma ya Luc Eymael kuibebesha Yanga tiketi ya CAF, kwani ushindi dhidi ya Kagera unaweza kuwatia ndimu na kukomaa kwa mechi zitakazofuata hadi fainali itakayopigwa baadaye wakati Ligi Kuu bara itakapokuwa imeshamalizika na bingwa kujulikana.

SAHARE NAO HATARI

Katika timu zilizotinga robo fainali ya safari hii, Sahare All Stars ndio pekee ya Daraja la Kwanza na inaonekana sio timu ya kubezwa, licha ya kwenye ligi yao ya FDL, hawana makali kivile.

Ilianza kwa kuishtukiza Panama ya Daraja la Pili kwa kuipiga mabao 5-5 kisha ikaitoa nishai Mtibwa Sugar kwa penalti 3-2 baada ya dakika 90 kuzimaliza wakiwa sare ya 1-1 na katika mechi ya raundi ya 16 wakaitungua timu ya Daraja la Kwanza, Njombe Mji kwa bao 1-0.

Safari hii wamepewa Ndanda ambayo inachechemea kwenye Ligi Kuu na moja ya klabu zilizo na hali mbaya kiuchumi na utamu ni kwamba kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo itacheza mechi ikiwa nyumbani. Mechi zao tatu zote za awali walipenya wakiwa viwanja vya ugenini.

Na hata ukiangalia njia waliyopita wao na wapinzani wao Ndanda utabaini Wana Kuchele ni lazima wajipange kama kweli wanataka kutinga nusu fainali na kuvaana ama na wapinzani wao wa Kanda ya Kusini, Namungo ama Alliance kutoka jijini Mwanza.

Kwa namna Sahare walivyozichanga karata zao tangu hatua ya awali ni wazi kwamba Ndanda ya Meja Abdul Mingange isipokaa vyema itawakuta kilichowakuta Mtibwa Sugar ya Zubeiry Katwila, ikizingatia Wagosi hao ndio wawakilishi pekee wa timu za Mkoa wa Tanga katika FA.

WATANI JASHO LITAWATOKA

Achana na kelele za mashabiki, Simba na Yanga zina vibarua vizito mbele ya wapinzani wao na ile kiu yao ya kutaka kuonyeshana umwamba baada ya kumalizana kwenye Ligi Kuu Bara.

Yanga inasaka tiketi ya kimataifa kupitia michuano hiyo, kwani hesabu kwenye Ligi Kuu zimekataa na watani zao Simba wamewazidi kete mapema. Simba ina kila dalili za kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu.

Yanga itapenda kuona inafuzu hadi fainali ili kujitengenezea mazingira ya kupata tiketi hiyo, lakini wapinzani wanaovaana nao Kagera Sugar sio wepesi kwani 3-0 walizowapa vijana wa Jangwani kwenye mechi ilioyokuwa ya kwanza kwa Kocha Luic Eymael ni salamu tosha kwao.

Simba ambao hesabu zao kutaka kuwatibulia watani wao na pia kutaka kuona wanawafunga mdomo ni lazima imalizane na Azam ambao waliwang’oa katika nusu fainali za msimu wa 2016-2017.

Azam imekuwa wakiisumbua Simba kwenye mechi za vikombe kama Kombe la Mapinduzi na hata kwenye ligi japo wamekuwa wanyonge kwa vijana wa Msimbazi, lakini hawezi kubezwa.

Kama Kagera na Azam zitaamua kupindua meza mashabiki wanaweza wasiione nusu fainali ya watani kama ilivyotokea msimu huu kwenye Kombe la Mapinduzi kwa Yanga kujipigisha shoti kwa Mtibwa na kurudi Dar na kuwaachia dhahama Simba ya kufunga fainali na Azam.

Je, ni Azam itakayolipa kisasi kwa Simba na kuendelea kulitetea taji lake, ama ni Simba itakayokuwa ikitaka kubeba mataji yote ya msimu huu, kwani tayari mkononi ina Ngao ya Jamii na ubingwa wa Ligi wanahesabu siku tu kwa alama ilizonazo kwenye msimamo? Tusubiri tuone!