KISHIKAJI : Cheki Arsenal, Juventus zinavyopeana tu mastaa

Muktasari:

  • Hawa hapa mastaa watano waliochezea kwenye vikosi vyote viwili vya Arsenal na Juventus ambao Ramsey atakwenda kufuata nyayo zao.

LONDON, ENGLAND.KIUNGO mshambuliaji wa Arsenal, Aaron Ramsey anajiandaa kujiunga na Juventus baada ya kudumu kwenye kikosi hicho cha Emirates kwa misimu 10.

Kwa muda wake aliokaa kwenye kikosi hicho, Ramsey hadi sasa ameshafunga mabao 61 katika mechi 354 na hakika amekuwa mchezaji muhimu kwa muongo mzima uliopita.

Na sasa anakwenda kujiunga na mabingwa wa Italia, ambao bila shaka atapata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza sambamba na masupastaa matata kabisa, Cristiano Ronaldo na Paolo Dybala.

Hata hivyo, Ramsey kama atafanikisha mpango wake wa kwenda kujiunga na Juventus kisha akapangwa kwenye mechi zake, hatakuwa mchezaji wa kwanza staa kuzitumikia timu hizo mbili kwenye mchezo huo wa soka baada ya wengine kibao kumtangulia kufanya hivyo.

Hawa hapa mastaa watano waliochezea kwenye vikosi vyote viwili vya Arsenal na Juventus ambao Ramsey atakwenda kufuata nyayo zao.

5.Nicolas Anelka

Nicolas Anelka amecheza kwenye klabu nyingi sana katika kipindi chake cha miaka 18 aliyodumu kwenye soka. Fowadi huyo wa Kifaransa amepachikwa jina la mzururaji. Katika timu alizocheza Anelka huko Ulaya, Arsenal na Juventus ni baadhi ya klabu hizo.

Anelka alijiunga na Arsenal mwaka 1997.

Kwenye kikosi hicho alifunga mabao 28 katika mechi 90 akicheza chini ya Kocha Arsene Wenger. Miaka miwili baadaye alikwenda kujiunga na Real Madrid, kisha akacheza Manchester City na Liverpool.

Kikosi cha Juventus alikichezea kwa mkopo katika msimu wa 2012-13. Kwenye Ligi Kuu England, kwenye klabu vigogo, Anelka hakucheza Manchester United tu, kwani alicheza hadi Chelsea.

4.Wojciech Szczesny

Szczesny ni kipa wa kimataifa wa Poland, ambaye aliichezea Arsenal kuanzia 2009 hadi 2017.

Alinaswa na Arsenal mwaka 2009 wakati huo ilipokuwa ikitafuta mrithi wa kudumu wa Jens Lehmann. Kiwango chake kilimfanya awe kipa namba moja kwenye kikosi hicho cha Arsenal na kuisaidia kubeba mataji ya Kombe la FA mwaka 2013-14 na 2014-15.

Kwa ujumla wake, aliichezea Arsenal mara 153. Baadaye alitolewa kwa mkopo kwenda AS Roma kuanzia 2015 hadi 2017, ambapo akabebwa jumla na Juventus na tangu wakati huo amekuwa akiwatumikia wababe hao wa Italia na tayari ameshabeba Serie A mara moja.

3.Stephan Lichtsteiner

Beki wa pembeni, Lichsteiner alinaswa na Arsenal kwenye dirisha lililopita la usajili wa majira ya kiangazi kuja kusaidiana na Hector Bellerin.

Beki huyo uzuri wake ni kwamba anaweza kucheza pande zote mbili za pembeni na hakika amekuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Unai Emery huko Emirates. Kabla hajasajiliwa na Arsenal, beki huyo alikuwa kwenye kikosi cha Juventus, ambacho alijiunga nacho mwaka 2011 na kuwa hapo hadi 2018.

Kwenye kikosi cha Juventus alifunga mabao 15 katika mechi 257 alizocheza huku akishinda mataji saba ya Serie A. Alikuwamo kwenye kile kikosi cha Juventus kilichoshika namba mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2014-15 na 2016-17.

2.Patrick Vieira

Patrick Vieira alikuwa supastaa matata kabisa kwenye kikosi cha Arsenal. Alikuwa kiungo mkabaji aliyeweza pia kujipa majukumu ya kucheza goli hadi goli.

Vieira alikuwa mchezaji mwenye nguvu ndani ya uwanja na kupiga pasi matata pia. Alikuwa nahodha wa Arsenal aliyewaongoza wenzake kwa mifano na hakika amekuwa akifahamika kama mmoja wa viungo matata kabisa waliowahi kutoka kwenye soka.

Vieira aliichezea Arsenal kutoka 1996 hadi 2005 na kufunga mabao 34 katika mechi 406. Alibeba mataji matatu ya Ligi Kuu England na baada ya hapo alienda zake Juventus mwaka 2005. Kwenye kikosi hicho cha Turin alicheza mechi 42 na kufunga mabao matano, lakini kwa bahati mbaya hakushinda taji lolote kabla ya kuondoka kwenda kujiunga na Manchester City.

1.Thierry Henry

Thierry Henry ni mmoja kati ya mastaa matata kabisa waliowahi kutokea kwenye kikosi cha Arsenal.

Baada ya fainali za Kombe la Dunia 1998 zilizofanyika Ufaransa, mwaka uliofuatia Henry alisajiliwa na Juventus na kwenda kucheza mechi kadhaa.

Kwenye kikosi hicho alikuwa akicheza kama winga na kufunga mabao matatu katika mechi 19. Lakini ndani ya mwaka huo huo, 1999, Henry alinaswa na Arsenal na kwenda kufanya kazi chini ya Arsene Wenger, ambaye alimbadilisha na kuanza kumtumia kama mshambuliaji wa kati. Jambo hilo lilimfanya Henry kutamba kwelikweli na kuwa gwiji kwenye kikosi hicho akiongoza kwa mabao.

Arsenal alicheza Arsenal hadi mwaka 2007, akifunga mabao 226 katika mechi 369. Alienda zake Barcelona kisha Marekani kabla ya kurudi tena Arsenal mwaka 2012 na kucheza mechi nne. Kwa ujumla wake, ameichezea Arsenal mara 373 na kufunga mabao 228.