KHA! Pogba, Man United yale yalee

Monday July 27 2020

 

MANCHESTER, ENGLAND. MPAKA dirisha la usajili linafungwa ni mengi yatasikika. Huko Old Trafford stori mpya ni kuhusu hatma ya kiungo wa Kifaransa, Paul Pogba. Awali, aliliweka bayana kuwa yuko tayari kuanza mazungumzo ya kusaini mkataba mpya wa miaka mitano kuendelea kubaki Old Trafford, lakini sasa ameanza tena kutikisa akizitaja Real Madrid na Juventus.

Pogba, ambaye msimu huu ameonekana mara chache kwenye kikosi cha kwanza cha Man United kutokana na majeraha, bado hakuna uhakika kama atabaki baada ya Madrid na Barcelona kuibuka upya kutaka saini yake.

Kwa sasa kiwango cha Pogba kimerejea kwenye ubora wake hasa baada ya kucheza sambamba na Bruno Fernandez, lakini haonekani kama ametulia kuendelea kubaki klabuni hapo msimu ujao. Hata hivyo, kama Pogba ataondoka basi atatoa fursa kwa mabosi wa United kuingia sokoni kunasa huduma za mastaa inaowataka akiwemo kiungo mshambuliaji wa Aston Villa, Jack Grealish na winga wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho.

Tayari, Dortmund inataka kulipwa Pauni 115 milioni huku United wakitangaza kuwa tayari kulipa pauni 50 milioni tu.

Lakini, kama Pogba atalazimisha kuondoka basi Man United itaweka dau la Pauni 130 milioni kwa timu inayomtaka ili kwenda kumaliza dili la Sancho.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ni shabiki mkubwa wa Pogba na amekuwa akimsaka usiku na mchana ili kwenda kucheza sambamba na Luka Modric na Toni Kroos.

Advertisement

Kwa upande wake Ole Gunnar Solskjaer alisema: “Tutaingia sokoni na mpango kabambe sana, kukisuka upya kikosi kwa ajili ya msimu ujao.”

Advertisement