KCB wamchukua kocha wa Wazito FC

Muktasari:

Ouna alijiunga na Wazito, ikiwa kwenye ligi daraja la kwanza, akaipandisha daraja kabla ya kuirudisha huko mchangani. Alikuwa msaidizi wa Frank Nuttal, ambapo kwa pamoja waliipatia Kogalo taji lao la 15 (2015/16). KCB wataanza kampeni yao kwenye KPL, dhidi ya Posta Rangers, Desemba 8, mwaka huu.

Nairobi, Kenya. Wageni wa ligi kuu ya Kenya (KPL), klabu ya KCB, wamemtangaza kocha wa zamani wa Wazito FC, Frank Ouna, kwa ajili ya msimu mpya wa unaotarajiwa kutimua kuanzia Desemba 8, mwaka huu.
Uamuzi wa kumchukua Ouna ambaye anachukua nafasi ya Elvis Ayany, ambaye alikuwa kocha wa muda baada ya Kocha John Kamau kuachia ngazi, umekuja baada ya klabu ya zamani ya Wazito FC kushushwa daraja. Ouna amesaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia klabu hiyo.
Ayany aliiongoza KCB kurejea kwenye ligi kuu ya Kenya, ambapo baada tu ya kukabidhiwa mikoba ya Kamau, aliisaidia KCB kushinda mechi sita mfululizo, ambayo iliwahakikishia nafasi ndani ya msimu ujao wa ligi kuu.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa mikoba ya kuinoa KCB, Ouna alisema atahakikisha mambo yaliyoitokea Wazito ambayo anasema alipambana kuinusuru, hayatatokea tena akiwahakikishia mashabiki wa klabu hiyo kwamba amekuja kushinda taji sio kushiriki.
"Hili ni jukumu jipya na kubwa zaidi. Najua kutakuwa na ugumu, lakini nimejipanga kuhakikisha tunapata matokeo katika kila mechi na ikibidi kutwaa ubingwa wa KPL. Nafahamu nina mzigo mkubwa mbele yangu, ila niwahakikishie kuwa nimekuja kufanya kazi,” alisema Ouna.