KAKOLANYA : Yanga mpya narudi golini

Muktasari:

  • Mwanaspoti limefanya naye mazungumzo kwa kirefu kuhusu maisha yake tangu amekaa nje ya uwanja, pamoja na mipango yake wakati akisubiri kupata barua ya kuwa huru kutoka katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

UTATA uliozunguka suala la Beno Kakolanya na klabu yake ya Yanga umemfanya kipa huyo kupotea midomoni mwa mashabiki wa soka kutokana na kukaa nje takribani miezi mitano bila kucheza.

Kakolanya alijiondoa katika kikosi cha Yanga baada ya kudai malimbikizo yake ya mshahahara na alipoambulia patupu aliamua kujiweka kando.

Kwa kujiweka kwake kando alijikuta akipoteza nafasi ya kuwa miongoni mwa nyota walioitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa kilichoshinda 3-0 mechi yao ya mwisho dhidi ya Uganda na kufuzu Afcon 2019, huku akiwa ni mlindamlango aliyetarajiwa kuwa msaidizi wa ‘Tanzania One’, Aishi Manula.

Mwanaspoti limefanya naye mazungumzo kwa kirefu kuhusu maisha yake tangu amekaa nje ya uwanja, pamoja na mipango yake wakati akisubiri kupata barua ya kuwa huru kutoka katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

MAISHA NJE YA YANGA FRESH TU

Kakolanya amekaa nje ya uwanja takribani miezi mitano tangu alipogoma kufanya kazi na Yanga, huku kesi yake ikiwa inapigwa danadana katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

Akipiga stori na Mwanaspoti juu ya maisha yake tangu akae nje ya Yanga, alisema jambo hila lina sura mbili katika maisha yake lakini kwa vile anajua nini anakifanya wala haliwezi kumsumbua.

“Siyo jambo zuri sana na wala siyo baya sana kwasababu lishatokea na lipo nje ya uwezo wangu kwasasa, kikubwa ni kuomba Mungu suala langu limalizike.”

Aliongeza kwamba amekuwa akifanya mazoezi madogomadogo ili kuhakikisha mwili unakaa sawa, kwani akikaa bila kufanya hivyo anaweza kupotea kabisa.

“Mwili wangu ulishaozea muda wote kufanya mazoezi magumu na mepesi kwahiyo siwezi kuuacha ukae hivihivi tu, ninachokifanya lazima niupe mazoezi ili uendelee kuwa fiti kwasababu ulishazoea mazoezi.”

WALA HANA PRESHA ASEE!

Kama ulikuwa unadhani baada ya kukaa nje kwa muda mrefu basi mchezaji huyu angeweza kukata tamaa ya kuendelea na soka, basi wala si hivyo, kwani Kakolanya anaamini bado ana nafasi kubwa ya kucheza.

“Muda wa kucheza bado upo. Nina umri mdogo sana na siwezi kukata tamaa kwa kipindi hiki, labda niamue mwenyewe tu kusema mpira basi, lakini bado nahitaji kucheza, hivyo naamini kabisa kwamba kila kitu kitawezekana.”

Akizungumzia timu ambayo anaipa kipaumbele kuichezea iwapo suala lake litamalizika mapema katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, alisema ni mapema mno kulizungumzia jambo hilo kutokana na hafahamu hatima yake mpaka hivi sasa.

MTAANI KIMYAA, MTANDAONI MH!

Jamaa huyu baada ya kuamua kuondoka Yanga, mashabiki wengi wamekuwa wakimpinga kwa kile alichokifanya na kuonekana kama msaliti katika klabu yao.

Lakini mwenyewe anafichua kwamba kwa upande wa mtaani kwake anapokaa, wananchi wengi mpaka wale mashabiki wa Yanga wanaelewa namna ambavyo alivyokuwa anaishi hivyo hawamghasi kuhusu kujiondoa Yanga.

“Kwa mtu ambaye haelewi na hafahamu hasa watu wa mitandaoni wao wanakuwa wanatukana tu muda wote, siwezi kuwajibu bali huwa naangalia halafu nacheka tu, lakini kwa upande wa mtaani kwangu wao wanaelewa wamekuwa wakinipa pole kila wanaponiona na huwa sipendelei kabisa kutokatoka nje basi nikitoka pole zinakuwa nyingi.”

AMSIKILIZIA AMUNIKE

Kipa huyu alikuwa ndiyo chaguo la pili katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kilichokuwa kinapambana na kutinga katika Fainali za Afcon 2019.

Lakini baada ya kujitoa Yanga, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, alimuondoa katika kikosi chake kilichocheza mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda jijini Dar es Salaam kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Kakolanya anawapongeza wachezaji wenzake kwa kile ambacho walikifanya huku kwa upande wake akishindwa kuzungumza kama anaweza kupata nafasi hata kama suala lake litamalizika.

“Sijatumika muda mrefu kwahiyo ni ngumu mno kuwa katika kikosi kitakachoenda Misri, lakini binafsi nimekuwa nikifanya mazoezi yangu na natamani kuendeleza safari niliyoanzisha na wenzangu, ikitokea nimeitwa nipo tayari kwasababu mazoezi nimekuwa nikifanya.”

POPOTE KAMBI TU

Kakolanya anafunguka jambo ambalo analisubiria kwa kipindi hiki ni kusikia tu maamuzi ya kamati ya sheria na hadhi ya wachezaji tu ili aweze kufanya maamuzi sahihi.

Alisema baada ya kutoka katika kikosi cha Yanga zilimfuata ofa nyingi kutoka nje ya nchi, lakini alishindwa kusaini kutokana na vuta ni kuvute iliyokuwapo katika kumueka huru.

“Sisi wachezaji hauwezi kuchagua kwamba hapa nitaenda hapa siendi kwasababu hii ni kazi yetu, kikubwa ambacho naweza kusema nchi yoyote kwangu mimi ni sawa tu lakini acha mambo yangu yaishe.”

Aliongeza kutokucheza kwake kunaweza kumfelisha kwa dili za nje, lakini anaamini akipewa muda wa wiki mbili tu za kufanya nao majaribio watamuelewa sana tu.

HESABU ZA KURUDI YANGA

Hivi sasa Yanga wapo katika michakato ya kuhakikisha wanapata viongozi wapya ambao wataiendesha timu hiyo kwa ubora kama ambavyo walivyo watani zao.

“Siwezi kukataa kwasababu naamini kabisa sina tatizo nao, bali waweke pesa mezani nitasaini na kuendelea na kazi yangu kama kawaida, inabidi itambulike mpira ni kazi kama kazi zingine.”

Usikose sehemu ya pili ya mahojiano haya kesho Jumatano akibainisha kuhusu uvumi wa kumwaga wino Simba.