Juventus wamwambia Sanchez shusha mshahara tukubebe

Muktasari:

  • Sanchez mwenyewe haonekani kuwa tayari kupoteza mshahara wake baada ya kusisitiza kwamba hatapenda kuondoka Man United kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa wachezaji

TURIN, ITALIA. JUVENTUS imemwambia Alexis Sanchez wapo tayari kumpa ofa ya kumwondoa kwenye majanga huko Manchester United, lakini kwanza itabidi akubali kushusha mshahara wake.

Tangu alipotua kwenye kikosi cha Man United, Sanchez mambo yake si mazuri kabisa, amekuwa akicheza chini ya kiwango na anaandamwa na majeruhi ya mara kwa mara.

 Huko Old Trafford, kocha Ole Gunnar Solskjaer ni kama anapiga hesabu za kumwondoa kikosini ili kupunguza bili ya mshahara wa Pauni 500,000 wanaomlipa staa huyo kwa wiki.

Lakini, Juve imemwambia itakuwa tayari kumfungulia njia ya kuondoka kwenye majanga hayo yanayomkabili huko Old Trafford, lakini kitu cha kwanza anachopaswa kufanya ni kukubali kupunguza mshahara.

Hata hivyo, Sanchez mwenyewe haonekani kuwa tayari kupoteza mshahara wake baada ya kusisitiza kwamba hatapenda kuondoka Man United kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa wachezaji.

Kwa mshahara mkubwa wanaomlipa Cristiano Ronaldo na ile wa Pauni 400,000 kwa wiki watakaokuja kumlipa Aaron Ramsey, Juventus hawahitaji kulipa tena mshahara mkubwa sana na ndio maana wanamtaka Sanchez kushuka ili wamnase.

Mabingwa hao wa Italia wanaamini Sanchez akitua kwenye kikosi chao atakwenda kucheza soka la kiwango cha juu na kurudi kwenye ubora wake. Fowadi huyo wa kimataifa wa Chile (30) mkataba wake na Man United umebakiza miaka mitatu.