Juve hawakomi kwa Paul Pogba

Muktasari:

  • Tangu Mourinho alipofutwa kazi Desemba mwaka jana, Pogba ameonyesha kiwango bora kabisa kwenye kikosi hicho tangu alipoanza kuwa chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer.

TURIN, ITALIA.JUVENTUS bado haitaki kabisa kusikia habari za kwamba wataachana na mpango wa kumfukuzia kiungo wa Manchester United, Paul Pogba.

Ripoti zinadai kwamba Pogba anapewa kipaumbele kikubwa na Juventus wakimtaka aende akaunde kombinesheni matata kwenye kiungo yao sambamba na Aaron Ramsey msimu ujao.

Kiungo huyo mwenye medali ya ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa, amerudi kwenye ubora wake kwa sasa huko Man United tangu timu hiyo ilipomfuta kazi kocha Jose Mourinho, aliyekuwa akilumbana naye mara kwa mara huko Old Trafford.

Tangu Mourinho alipofutwa kazi Desemba mwaka jana, Pogba ameonyesha kiwango bora kabisa kwenye kikosi hicho tangu alipoanza kuwa chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer. Lakini, Juventus wao hawataki kabisa kufunga mjadala wa kumnasa mchezaji huyo na mpango ni kwamba mwisho wa msimu wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa, basi watapambana na Man United kumnasa supastaa huyo.

Juve wao wameshakamilisha mpango wa kumchukua kiungo wa Arsenal, Ramsey, atakayejiunga na timu hiyo bure kutokana na mkataba wake kufika mwisho huko Emirates na mabingwa hao wa Serie A wanamtaka Pogba akawe pacha wake.