Junior achekelea kumtungua Kaseja

Sunday October 25 2020
waziri jr pic

STRAIKA mpya wa Yanga, Waziri Junior ameweka wazi kwamba kitendo cha kufunga bao la ushindi dhidi ya KMC katika ushindi wa 2-1 ametengeneza rekodi mpya ya kumfunga Juma Kaseja.

 

Akizungumza baada ya mpira kumalizika, Junior amesema katika katika maisha yake ya soka hakuwahi kumfunga Kaseja, hivyo leo katika mchezo huo alikuwa ameweka nia ya kumfunga kipa huyo.

 

"Tangu nianze kucheza Ligi nimecheza mechi 60 na kufunga magoli 34 lakini sikuwahi kumfunga Kaseja, leo wakati natoka chumbani nilimwambia Makapu (Said) kwamba leo nafunga hapa na imekuwa hivyo."

 

Advertisement

Junior ambaye baada ya kufunga bao hilo kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyopigwa na Farid Mussa alivua jezi yake na kubakiwa na singlendi iliyoandikwa “The King of the CCM Kirumba” alifunguka zaidi kwa kusema kufunga kwake bao hilo la kwanza kwake kwa msimu huu, utakuwa ni muendelezo katika mechi zijazo.

 

"Sikupata nafasi ya kucheza mechi sita za nyuma, hii ni mechi yangu ya kwanza na nimefanikiwa kufunga ni jambo zuri kwangu."

 

Kwa upande wa kocha mkuu wa Yanga, Cedric Kaze akizungumzia kiwango cha mchezaji wake, alisema mchezaji huyo anamfanya kuwa na machaguo mengi anapokuwa yupo uwanjani.

 

"Junior ni mchezaji ambaye anaweza kucheza kama mshambuliaji wa kusimama lakini pia kama mshambuliaji wa pili ambaye anakuja kuchukua mipira chini, anapokuwa uwanjani ananipa machaguo mengi."

Advertisement