Juma Nature amchana Molinga

Muktasari:

Nature ambaye ni shabiki wa Yanga alisema kila anapopangwa Molinga kucheza, amekuwa akiona anajiangusha na kulalamika

MSANII wa Bongofleva, Sir Juma Nature amemchana straika wa Yanga, David Molinga kuachana na tabia yake ya kujiangusha angusha uwanjani badala ya kupambana kuisaidia timu yake kupata ushindi.

Nature ambaye ni shabiki wa Yanga alisema kila anapopangwa Molinga kucheza, amekuwa akiona anajiangusha na kulalamika, jambo linalomkera nakuona haendani na mwili wake.

Alisema Molinga ana mwili mpana wakumuwezesha kupambana na mabeki, lakini anastajabishwa kuona mara nyingi ananyosha nyosha mkono kwa refa kulalamika.

“Tabia yake ya kujiangusha angusha, anakuwa anawapa uvivu viungo kupambana na kumtengenezea nafasi ya kufunga, tofauti na mchezaji anapokuwa anapambana kusaka nafasi za kufunga, basi viungo wanakuwa wanakasi ya kumpa mipira,”

Aliongeza “Mfano alipokuwepo Donald Ngoma kabla ya kwenda Azam FC, alikuwa mpambanaji kiasi viungo walikuwa wanajituma kumtengenezea nafasi za kufunga, mpaka alikuwa anawafanya mabeki wanamchezea rafu ambazo zilikuwa zinafaida kwa Yanga.”

Alisema hana maana Molinga akiumizwa asilalamike, ila isiwe kwa kujiendekeza kwasababu soka ni ushindani, wakati mwingine nguvu inatakiwa itumike kulazimisha mashambulizi.

“Soka lina mbinu nyingi, mfano timu pinzani inaongoza wakikugundua unapenda kujiangusha ovyo wanakuwa wanafanya kusudi, huku muda unakuwa unazidi kwenda, mnajikuta mnapoteza, lakini kama mnapambana basi matokeo yatapatikana,” alisema.

Alisema amecheza soka ndio maana anatambua yapo makosa, Molinga anajiangusha bila sababu, bila kujua anakuwa anapunguza kasi ya upambanaji.

“Dakika 90 zinakuwa za mapambano, hivyo si busara hata kitu kidogo unakuwa unahitaji kusaidiwa, nimemtaja Molinga kwa sababu yupo kwenye timu ninayoipenda, nje na hapo wapo wengi ambao wanafanya tuboreke badala ya kufurahia burudani.”