Joto lazidi kupanda mechi ya Yanga, Coastal Union

Muktasari:

Mashabiki wa Coastal akiwepo Juma Kiondo pamoja na Rashid Karim walisema kupoteza mchezo uliopita wala haiwatii shaka kuelekea mchezo wao na Yanga wanachioamini ni kuwa lazima Yanga atakaa mbele yao

TAMBO za mashabiki wa Wagosi wa Kaya, Coastal Union na Yanga zimezidi kunoga na sasa kinachosubiriwa ni kuona kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini hapa nini kitatokea baina ya timu hizo zitakapocheza mechi ya Ligi Kuu Bara.
Tambo za mashabiki hao ni kutokana na rekodi za timu zote mbili walizozipata kwenye michezo iliyopita ambapo Coastal Union wao walipoteza mbele ya Ruvu Shooting mabao 2-1 huku Yanga nao wakilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania walipocheza Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Rekodi hizo zinawafanya mashabiki wao kuzungumza kwa kujiamini kila mmoja akiipa timu yake asilimia kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo kitu ambacho kinaashiria kuwa mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa.
Mashabiki wa Coastal akiwepo Juma Kiondo pamoja na Rashid Karim walisema kupoteza mchezo uliopita wala haiwatii shaka kuelekea mchezo wao na Yanga wanachioamini ni kuwa lazima Yanga atakaa mbele yao.
“Yanga tunawafahamu wanakata upepo mapema lazima tuchukue pointi tatu mbele yenu wala hilo halina upinzan,” walitamba mashabiki hao
Upande wa mashabiki wa Yanga nao wanasema kuhusu ushindi wa timu yao siku hiyo  ni lazima kwa madai kwamba Coastal ni sawa na wadogo zao.
Yanga ambao wana mechi mbili za viporo mkononi wanaingia uwanjani wakiwa na pointi 40 na kusimama nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakati Coastal wenyewe wapo nafasi ya tano wakiwa na pointi 38.